Lugha Nyingine
Iran yalaani mashambulizi mapya ya Marekani kwenye majimbo ya kusini na madaraja
TEHRAN - Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mashambulizi mapya ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya maeneo kadhaa katika majimbo ya pwani ya kusini mwa Iran na madaraja mawili katika majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Katika taarifa yake jana Alhamisi, wizara hiyo imeyaelezea mashambulizi hayo kwenye madaraja mawili katika njia za reli kutoka Gorgan hadi Incheh Borun na Mashhad hadi Tehran kuwa ni "uhalifu wa kivita wa waziwazi."
Imesisitiza kwamba mashambulizi hayo ya Marekani ndani ya saa 48 zilizopita, yaliyofanywa chini ya "kisingizio cha uwongo" cha kujibu matukio ya awali yaliyohusisha meli zinazovuka Mlango-Bahari wa Hormuz, ni katika kukiuka waziwazi Katiba ya Umoja wa Mataifa na hati ya makubaliano (MoU) iliyotiwa saini hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili juu ya kumaliza vita. Wizara hiyo pia imeishutumu Marekani kwa kutumia mashambulizi hayo kuhalalisha "kuendelea kwake kutokufuata" MoU.
Akizungumzia mashambulizi hayo ya Marekani, Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf amesema katika ujumbe wake wa Alhamisi kwenye mtandao wa kijamii wa X, "Marekani bado haijajifunza kwamba umwamba na uvunjaji wa ahadi siyo tena bila gharama."
Ameonya kwamba kama Marekani itaipiga Iran, itapokea vipigo, akisisitiza kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa tu kwa mipangilio ya Iran, na si kwa vitisho vya Marekani.
Kamandi ya Mashariki ya Kati ya Jeshi la Marekani ilisema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X mapema Alhamisi kwamba vikosi vyake vimekamilisha raundi ya nyongeza ya mashambulizi dhidi ya Iran ili "kupunguza zaidi uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara na mabaharia wa kiraia wasio na hatia katika Mlango-Bahari wa Hormuz," yakiwa ni siku ya pili mfululizo ya hatua hiyo.
Katika kulipiza kisasi, IRGC na jeshi la Iran wamesema wameshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Kuwait, Bahrain na Qatar.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



