Lugha Nyingine
Uganda yamruhusu kuondoka mgonjwa wa mwisho wa Ebola, yaanza kuhesabu siku 42 kumaliza mlipuko

Waziri wa Afya wa Uganda Chris Baryomunsi (katikati) akizungumza na vyombo vya habari kwenye Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago jijini Kampala, Uganda, Julai 16, 2026. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA - Uganda imemruhusu kuondoka hospitalini mgonjwa wake wa mwisho wa Ebola jana Alhamisi baada ya mtu huyo kupimwa na kukutwa hana virusi hivyo, ikiashiria kuanza rasmi kwa kuhesabu siku 42 ili kuutangaza mlipuko huo kuisha nchini humo, kama hakuna maambukizi mapya yatakayobainika katika kipindi hicho.
Waziri wa Afya wa Uganda Chris Baryomunsi aliongoza hafla ya kiishara ya kumruhusu mgonjwa huyo kuondoka hospitalini kwenye Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago katika mji mkuu, Kampala.
Kwenye hafla hiyo, Baryomunsi alimpa mgonjwa huyo cheti cha kuruhusiwa kuondoka hospitalini cha Ebola akisema kwamba hana hatari tena ya kusambaza virusi hivyo baada ya kupimwa na kukutwa hana virusi.
"Hali yake ya sasa ya kiafya haisababishi hatari kwa jamii na kwa hivyo anaweza kurudi katika mazingira yake ya nyumbani na kitaaluma na kuendelea na shughuli zake za kawaida," waziri huyo amesema.
"Jamii na mamlaka zinaombwa kumkubali ili kuhamasisha ujumuishwaji wake kijamii," ameongeza.
Kasonde Mwinga, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Uganda, amesema nchi hiyo iliweza kudhibiti mlipuko huo kutokana na kujiandaa kwake, akibainisha kuwa timu za kukabiliana na Ebola zilikuwa katika hali ya tahadhari kubwa wakati wote wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Mwinga amesema kujiandaa kwa nchi hiyo pia kumesaidia kudhibiti kiwango cha vifo chini ya asilimia 10, moja ya rekodi za chini kabisa katika milipuko ya Ebola.
Kwa mujibu wa WHO, nchi inaweza kutangaza kuisha kwa mlipuko wa Ebola baada ya siku 42 mfululizo bila maambukizi mapya yaliyothibitishwa kufuatia tarehe ambapo mgonjwa wa mwisho aliyethibitishwa hana uwezo tena wa kusambaza virusi hivyo.
Amesema hiyo hutokea pale mgonjwa anapokuwa ama amepona, kupimwa na kukutwa hana virusi na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, au kufariki. Ameeleza, kama hakuna maambukizi mapya yaliyothibitishwa wakati wa kipindi cha siku hizo 42, mlipuko huo hutangazwa rasmi kuisha.
Uganda ilitangaza mlipuko wa Ebola Mei 15 baada ya mgonjwa aliyekuwa amesafiri kutoka mashariki mwa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kitovu cha mlipuko wa sasa, kupimwa na kukutwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Tangu wakati huo, nchi hiyo imerekodi watu 20 waliothibitishwa kuambukizwa, wakiwemo raia 15 wa DRC na Waganda watano. Wawili kati ya wagonjwa hao walioambukizwa walifariki.

Wafanyakazi wa matibabu wakimruhusu kuondoka mgonjwa wa mwisho wa Ebola (kulia, mbele) kwenye Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago jijini Kampala, Uganda, Julai 16, 2026. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

Picha iliyopigwa Julai 16, 2026 ikionyesha Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago jijini Kampala, Uganda. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



