Meli hospitali ya Kikosi cha Majini cha China yaanza safari ya kutoa huduma ya matibabu ya kibinadamu katika Afrika, Asia Kusini (2)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 23, 2026
Meli hospitali ya Kikosi cha Majini cha China yaanza safari ya kutoa huduma ya matibabu ya kibinadamu katika Afrika, Asia Kusini
Meli hospitali ya Kikosi cha Majini cha Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA), Auspicious Ark, ikiondoka kutoka bandarini mjini Qingdao, Mkoa wa Shandong, mashariki mwa China, Julai 22, 2026. (Picha na Liu Zaiyao/Xinhua)

QINGDAO - Meli hospitali ya Kikosi cha Majini cha Jeshi la Ukombozi wa Umma la China (PLA), Auspicious Ark imeondoka kutoka bandarini mjini Qingdao, Mkoa wa Shandong mashariki mwa China, jana Jumatano kwa ajili ya jukumu la kutoa huduma ya matibabu ya kibinadamu barani Afrika na Asia Kusini.

Safari hiyo ambayo imepewa jina la Mission Harmony-2026, ambayo ni ya 12 katika mfululizo wa safari za Mission Harmony zilizoanza tangu mwaka 2010, imepangwa kudumu kwa siku zaidi ya 200, ambapo meli hiyo itatembelea nchi mbalimbali za Afrika na Asia Kusini ili kutoa huduma za matibabu bila malipo kwa wakazi wenyeji.

Askari na wafanyakazi ndani ya meli hiyo pia watafanya mabadilishano ya kitamaduni na nchi husika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Ulinzi wa Taifa ya China, mpango huo unalenga kuimarisha urafiki wa jadi na ushirikiano wa kivitendo kati ya China na nchi husika, kuipa jumuiya ya kimataifa bidhaa zaidi za usalama wa umma, kutekeleza vyema Pendekezo la Usalama Duniani, na kuchangia katika kujenga jumuiya ya mambo ya baharini yenye mustakabali wa pamoja.

Meli hiyo yenye idara 18 za kliniki na vitengo vitano vya kusaidia upimaji na utambuzi wa magonjwa, ina uwezo wa kufanya aina zaidi ya 60 za uchunguzi wa tiba, matibabu na taratibu zinazohusisha upasuaji wa jumla, mifupa, uzazi na magonjwa ya wanawake, magonjwa ya macho na zaidi. Vyumba vyake vinane vya kiwango vya upasuaji ndani ya meli vinawezesha kufanya upasuaji mbalimbali kwa wakati mmoja, na helikopta ndani ya meli hiyo inaongeza uwezo wake wa uokoaji wa kimatibabu wa dharura.

Safari hiyo ni jukumu la kwanza la nje ya nchi kwa Auspicious Ark, meli ya tatu ya hospitali ya baharini inayosanifiwa na kuundwa ndani ya China yenye tani 10,000.

Timu hiyo ya matibabu yenye watu zaidi ya 100 imeundwa hasa na wafanyakazi wa kimatibabu kutoka Kikosi cha Majini cha Eneo la Kivita la Kaskazini la PLA, pamoja na wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Kikosi cha Majini na vitengo vingine.

Mbali na kutoa matibabu ndani ya meli, wafanyakazi hao wa matibabu pia watatumwa kama timu za kuhama hama kutoka eneo moja hadi lingine kwa ajili ya kutoa huduma za kimatibabu kwa jamii za wenyeji.

Meli hiyo mpya kabisa ya Auspicious Ark iliyozinduliwa mwaka 2025, ina vifaa karibu vyote vya kimatibabu vya kisasa vinavyopatikana katika hospitali ya kiwango cha juu, hali ambayo inaiwezesha kutoa huduma bora ya kimatibabu katika mazingira mbalimbali. Tangu wakati huo imeshiriki katika mazoezi kadhaa ya uungaji mkono wa matibabu ya baharini.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha