Kiasi cha mizigo cha reli ya SGR ya Kenya chazidi tani milioni 50

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 28, 2026
Kiasi cha mizigo cha reli ya SGR ya Kenya chazidi tani milioni 50
Treni ya mizigo ikionekana katika Stesheni ya Reli ya Port Reitz kwenye ya Reli ya Standard Gauge (SGR) ya Mombasa-Nairobi, Mombasa, Kenya, Julai 9, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)

NAIROBI - Kiasi cha jumla cha mizigo kilichosafirishwa kwenye ya Reli ya Standard Gauge (SGR) ya Mombasa-Nairobi ya Kenya, mradi kinara chini ya ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), kimezidi tani milioni 50 kufikia Julai 26, Kampuni ya Uendeshaji wa Reli ya Africa Star (Afristar) imesema Jumatatu.

Kampuni hiyo imesema tangu kuanza kwa uendeshaji wake Mei 31, 2017, reli hiyo ya SGR ya Mombasa-Nairobi imedumisha rekodi ya uendeshaji salama kwa siku zaidi ya 3,300 mfululizo.

Kampuni hiyo ambayo inatoa uungaji mkono wa kiutendaji na kiufundi kwa SGR ya Mombasa-Nairobi imesema katika kipindi hicho, reli hiyo imesafirisha abiria jumla ya milioni 18.606, wakati jumla ya mizigo ikiwa imefikia tani milioni 50.015.

Reli hiyo ina urefu wa kilomita 472, ikiunganisha jiji la bandari la Mombasa katika sehemu ya kusini-mashariki mwa nchi hiyo na mji mkuu, Nairobi. Ni reli ya kwanza ya kisasa iliyojengwa nchini Kenya tangu ipate uhuru wake na inasimama kama mafanikio muhimu ya ushirikiano kati ya China na Kenya chini ya BRI.

Tangu huduma za mizigo zianze rasmi mwaka 2018, kiasi cha mizigo kimeendelea kuongezeka, wakati huohuo ufanisi wa uendeshaji umeimarika kwa kasi.

Huduma ya mizigo ya SGR ambayo hapo awali ilikuwa ikisafirisha mizigo iliyo kwenye kontena zaidi, sasa imepanuka hadi kujumuisha aina mbalimbali kama vile nafaka, mbolea, chuma, klinka ya saruji, bidhaa za kilimo, na mizigo ya mnyororo wa baridi.

Reli hiyo imeboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wa uchukuzi, kupunguza gharama za jumla za usafirishaji, kuimarisha muunganisho kati ya Bandari ya Mombasa na maeneo ya ndani ya bara, na kusaidia kuhakikisha uendeshaji tulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji.

Kampuni hiyo ya Afristar imesema itaendelea kufanya kazi na Shirika la Reli la Kenya ili kuongeza uwezo wa usafiri na ubora wa huduma, kutoa huduma za reli zenye ufanisi, salama na rahisi zaidi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Kenya.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha