Italia na Saudi Arabia zasisitiza uungaji mkono kwa suluhisho la nchi mbili, kusimamisha mapigano Gaza (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 30, 2026
Italia na Saudi Arabia zasisitiza uungaji mkono kwa suluhisho la nchi mbili, kusimamisha mapigano Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud, Naibu Waziri Mkuu wa Italia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Antonio Tajani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Varsen Aghabekian Shahin (kutoka kushoto hadi kulia) wakihudhuria mkutano wa Muungano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Suluhisho la Nchi Mbili jijini Roma, Italia, Julai 29, 2026. (Xinhua/Wang Kaiyan)

ROME - Italia na Saudi Arabia jana Jumatano zimesisitiza uungaji wao mkono kwa utekelezaji wa suluhisho la nchi mbili kwa mgogoro kati ya Israel na Palestina, zikitoa wito wa usimamishaji wa mapigano Gaza udumishwe, usaidizi wa kibinadamu uongezwe na juhudi za kuelekea amani ya kudumu zifanywe upya tena.

Wito huo umetolewa katika tamko la pamoja lililotolewa baada ya mazungumzo kati ya Naibu Waziri Mkuu wa Italia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Antonio Tajani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud wakati wa mkutano wa Muungano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Suluhisho la Nchi Mbili, uliofanyika Roma, Italia Julai 28-29.

Mawaziri hao wawili wamekaribisha matokeo ya mkutano wa muungano huo na kusisitiza uungaji wao mkono kwa utekelezaji wa Azimio namba 2803 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mpango Jumuishi wa Kumaliza Mgogoro wa Gaza.

Wamesisitiza hitaji la kudumisha usimamishaji mapigano huko Gaza, kuondoa mambo ya kijeshi katika Ukanda huo, kuhakikisha usaidizi wa kibinadamu unasafirishwa bila vizuizi, kuanzisha juhudi za mapema za ujengaji upya na kuunga mkono mageuzi ya Mamlaka ya Palestina.

Tamko hilo pia limelaani kupamba moto kwa vurugu za walowezi katika Ukingo wa Magharibi, likisisitiza upingaji dhidi ya aina yoyote ya uchukuaji ardhi au kuwahamisha kwa lazima Wapalestina, na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwemo sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Pande hizo mbili pia zimejadili usalama wa baharini katika Bahari Shamu na Mlango-Bahari wa Hormuz, hali nchini Yemen, usalama wa chakula wa kikanda na ushirikiano wa pande mbili. Zimeahidi kuendelea kuratibu juhudi za kuhimiza amani na utulivu wa kikanda na kusukuma mbele suluhisho la nchi mbili.

Muungano huo wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Suluhisho la Nchi Mbili uliozinduliwa mwezi Septemba 2024, unalenga kuratibu juhudi za kimataifa za kisiasa, kiusalama, kibinadamu na kiuchumi ili kusukuma mbele suluhisho la nchi mbili na hutumika kama jukwaa la ufuatiliaji kwa mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo wa Roma ulileta pamoja wajumbe kutoka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Japani, Saudi Arabia, Jordan, Qatar, Canada na Brazil, vilevile wawakilishi wa Palestina na Umoja wa Mataifa, kujadili njia za kusukuma mbele mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha