Lugha Nyingine
Hispania yaweka kizuizi cha baharini kikamilifu wakati idadi ya vifo kutokana na mgogoro wa wahamiaji la Ceuta ikiongezeka

Watu waliokusanyika kwenye upande wa Morocco wa mpaka na eneo la Ceuta la Hispania la Afrika Kaskazini, wakijiandaa kuvuka kuingia katika eneo hilo, Julai 30, 2026. (Picha na Liu Wenyong/Xinhua)
MADRID - Hispania imeweka kizuizi cha baharini kikamilifu jana Jumapili kwenye mpaka wa baharini wa eneo lake la Ceuta la Afrika Kaskazini wakati mamlaka zikiendelea kuimarisha udhibiti wa mpaka kufuatia wimbi la hivi karibuni la wahamiaji wengi kutoka Morocco.
Kizuizi hicho kinachoelea, kilichowekwa karibu na ufukwe wa Tarajal wa Ceuta, sasa kinafanya kazi kabisa. Hatua hiyo imewekwa ili kuzuia uvukaji wa baharini usiofuata utaratibu baada ya makumi ya maelfu ya wahamiaji kuingia kwenye eneo hilo katika siku za hivi karibuni, ambao wengi wao waliingia kwa kuogelea.
Mamlaka za Hispania zimesema siku hiyo ya Jumapili kwamba idadi rasmi ya vifo vinavyotokana na janga hilo imeongezeka hadi 72.
Wakati huo huo, serikali ya eneo hilo la Ceuta imesema miili 88 kwa sasa inahifadhiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti cha mji huo. Mamlaka za serikali za mtaa zimesema baadhi ya miili hiyo iliopolewa baharini wiki zaidi ya mbili baada ya ongezeko kubwa la wahamiaji. Zimesema mchakato wa utambuzi bado unaendelea.
Ingawa idadi kubwa ya waliowasili imepungua, Ceuta bado haijarejea katika hali ya kawaida. Polisi na wanajeshi waliendelea na operesheni za usalama kote katika mji huo jana Jumapili, na kushikilia wahamiaji walioonekana mitaani.
Wale waliokamatwa walipelekwa vituo vya polisi kwa ajili ya utambuzi kabla ya taratibu za kufukuzwa nchini humo kuanza.
Ongezeko hilo la wahamiaji limekuwa moja ya migogoro mikubwa zaidi ya mpaka katika historia ya hivi karibuni ya Hispania, hali ambayo imesababisha hatua za dharura kuchukuliwa na serikali ya Hispania na kuibuwa mjadala mpya kote Ulaya juu ya usimamizi wa uhamiaji na ulinzi wa mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya.

Wahamiaji wasiofuata utaratibu wakiwa wamekusanyika nje ya duka la kuuza vitu vya matumizi katika eneo la Ceuta la Hispania, Afrika Kaskazini, Julai 30, 2026. (Picha na Liu Wenyong/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



