Majimbo 25 ya Marekani yaushtaki utawala wa Trump juu ya ushuru wa Kifungu cha 301

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 04, 2026

Picha iliyopigwa Aprili 15, 2026 ikionyesha gati la makontena la Bandari ya New York na New Jersey, ambalo hutumika kama lango muhimu la biashara na kitovu kikubwa cha uchukuzi kwa kaskazini-mashariki mwa Marekani, New York, Marekani. (Xinhua/Zhang Fengguo)

Picha iliyopigwa Aprili 15, 2026 ikionyesha gati la makontena la Bandari ya New York na New Jersey, ambalo hutumika kama lango muhimu la biashara na kitovu kikubwa cha uchukuzi kwa kaskazini-mashariki mwa Marekani, New York, Marekani. (Xinhua/Zhang Fengguo)

NEW YORK – Muungano wa majimbo 25 umewasilisha kesi dhidi ya utawala wa Trump jana Jumatatu, ukisema kwamba Rais wa Marekani Donald Trump amezidi mamlaka yake ya kisheria kwa kuweka ushuru mkubwa mpya kwa bidhaa kutoka kwa washirika 60 wa biashara, kwa mujibu wa hati ya mahakama.

Malalamiko hayo, yaliyowasilishwa katika Mahakama ya Biashara ya Kimataifa ya Marekani, yanapinga ushuru uliopitishwa hivi karibuni wa asilimia 10 au asilimia 12.5 kwa idadi kubwa ya bidhaa zinazoagizwa kutoka kwa nchi zinazoathiriwa. Kwa mujibu wa majimbo hayo, nchi hizo kwa pamoja zinachukua asilimia 99.4 ya uagizaji wote bidhaa wa Marekani.

Muungano huo unaiomba mahakama kuzuia ushuru huo, kuutangaza kuwa ni kinyume cha sheria, na kutoa amri ya kurejeshwa kwa ushuru ambao tayari umelipwa.

Shtaka hilo linafuatilia juhudi za utawala huo kuhifadhi mfumo mkubwa wa ushuru wa Trump baada ya mahakama kuu kukataa matoleo mawili ya awali yaliyowekwa chini ya mifumo tofauti ya kisheria.

Majimbo hayo yanasema kwamba maafisa wa serikali kuu walichukua Kifungu cha 301 cha Sheria ya Biashara ya 1974 na wasiwasi wa utumikishaji kazini kwa lazima kama kisingizio cha kuleta upya kwa haraka ushuru duniani unaofanana na uleule wa awali ambao Mahakama Kuu iliufuta hapo awali mwezi Februari.

"Ushuru huo haramu wa Rais Trump si chochote zaidi ya kodi kwa familia zinazofanya kazi kwa bidii, unaongeza gharama za manunuzi ya mahitaji, vitu muhimu vya nyumbani, vifaa vya ujenzi, na bidhaa nyingi za kila siku ambazo wakazi wa New York wanategemea," amesema Gavana wa New York Kathy Hochul katika taarifa.

"Baada ya kushindwa katika Mahakama Kuu, utawala unajaribu tena kuongeza ushuru kinyume cha sheria kwa familia na biashara kwa raundi mpya ya ushuru," Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James amesema.

Ikulu ya White House imekataa hoja za muungano huo wa majimbo, ikidai kwamba ushuru wa Kifungu cha 301 umethibitika kuwa "chombo cha kudumu kisheria" tangu muhula wa kwanza wa rais na unabaki hivyo chini ya utawala wa sasa.

Majimbo mengine yanayoungana na New York katika kesi hiyo iliyotangazwa Jumatatu ni Arizona, California, Colorado, Connecticut, Delaware, Hawaii, Illinois, Kentucky, Massachusetts, Maryland, Maine, Michigan, Minnesota, Nevada, New Jersey, New Mexico, North Carolina, Oregon, Pennsylvania, Rhode Island, Virginia, Vermont, Washington na Wisconsin. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha