Lugha Nyingine
Kampuni ya China yazindua mpango wa kukuza vipaji kuchochea maendeleo ya miundombinu ya Cameroon

Wageni wakipiga picha ya pamoja na wanafunzi wa kozi ya mafunzo baada ya hafla ya uzinduzi, Yaounde, Cameroon, Agosti 3, 2026. (Xinhua/Kepseu)
YAOUNDE – Kampuni ya Uhandisi ya First Highway ya China (CFHEC) imezindua mpango wa mafunzo uliopewa jina la Mpango wa Vipaji wa Seagull jana Jumatatu ili kujenga utaalamu wa wenyeji nchini Cameroon.
Mpango huo umezinduliwa katika mji mkuu, Yaounde, ambapo maafisa waandamizi wa serikali ya Cameroon, wanadiplomasia wa China, walimu kutoka Shule ya Juu ya Kitaifa ya Kazi za Umma (ENSTP), na wanafunzi walihudhuria.
Kozi hiyo ya siku 10 inawaleta pamoja washiriki 54, wakiwemo wafanyakazi 24 wenyeji wa mradi na wanafunzi 30 wa ENSTP.
Mafunzo hayo, yanayotolewa na watathmini wataalamu wa China na wahadhiri wa ENSTP, yanahusu nadharia ya upimaji, uendeshaji wa vifaa, na mazoezi ya kivitendo, pamoja na moduli juu ya utamaduni wa kampuni na uendeshaji wa droni.
Yang Song, meneja mkuu wa kitengo cha shughuli za kimataifa cha CFHEC, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kuwa "kizalishi cha vipaji."
"Kupitia utaratibu wa mafunzo uliopangwa na wa hatua kwa hatua, Mpango wa Vipaji wa Seagull unalenga kuongeza ujuzi wa kitaalamu na uwezo wa kufanya kazi kama timu wa wafanyakazi wenyeji kila wakati, na kujenga nguvu kazi yenye mtazamo wa kimataifa, utaalamu imara wa kiufundi, na ujuzi wa mawasiliano kati ya tamaduni," Yang amesema.
"Pia unaimarisha rasilimali watu zinazohitajika kwa mkakati wetu wa kimataifa na unaongeza kasi kwenye maendeleo ya miundombinu na maendeleo ya kisasa nchini Cameroon," Yang ameongeza.
Waziri wa Elimu ya Juu wa Cameroon Jacques Fame Ndongo ameuelezea mpango huo kuwa ni uhamishaji wa moja kwa moja wa ujuzi na teknolojia unaoendana na lengo la serikali la kuifanya elimu kuwa ya kitaalamu.
"Mnafungua ofisi zenu za usanifu na maeneo ya ujenzi kwa wanafunzi wetu, kusaidia kuoanisha mitaala yetu ya vyuo vikuu na viwango vya kimataifa, na kuingiza teknolojia na viwango vinavyotumika katika miradi mikubwa ya China. Hiki ni kitendo cha imani kwa vijana wa Cameroon," Ndongo amesema.
Mafunzo hayo yameidhinishwa na kutolewa vyeti kwa pamoja na Wizara ya Elimu ya Juu ya Cameroon, CFHEC, na Jumuiya ya Barabara Kuu na Usafiri ya China.
CFHEC imekuwa ikifanya shughuli zake nchini Cameroon tangu mwaka 1992. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, imekamilisha miradi ya miundombinu karibu 132 na kutoa mafunzo kwa wataalamu wenyeji zaidi ya 2,000 kwenye taaluma tofauti katika kipindi hicho.

Kundi la kwanza la wanafunzi wa kozi ya mafunzo wakihudhuria hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Vipaji wa Seagull, Yaounde, Cameroon, Agosti 3, 2026. (Xinhua/Kepseu)

Waziri wa Elimu ya Juu wa Cameroon Jacques Fame Ndongo akihutubia hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Vipaji wa Seagull, Yaounde, Cameroon, Agosti 3, 2026. (Xinhua/Kepseu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



