Lugha Nyingine
China yalenga uzalishaji wa umeme kwa nishati zisizo za visukuku wa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030

Picha iliyopigwa Julai 6, 2026 ikionyesha hali ya kituo cha Dongshan Xingchen cha kuzalisha umeme wa megawati 180 kwa nishati ya jua baharini cha Kundi la Magenge Matatu la China huko Zhangzhou mkoani Fujian, kusini mashariki mwa China. (Xinhua/Lin Shanchuan)
BEIJING – Kutokana na mpango mpya wa kitaifa, yaani mpango wa malengo ya maendeleo ya sekta ya nishati ya China ya kipindi cha mwaka 2026-2030, sehemu ya umeme wake unaozalishwa kwa nishati zisizo za visukuku itaongezwa kuwa ya asilimia 50.
Mpango huo wa miaka mitano uliotolewa kwa pamoja na Kamati ya Maendeleo na Mageuzi ya Kitaifa ya China na Mamlaka ya Nishati ya Kitaifa ya China, unaweka dira ya jumla kwa sekta ya umeme ya China katika kipindi cha 2026-2030 na unalenga kuanzishwa kwa hatua ya kwanza kwa mfumo mpya wa umeme ifikapo mwaka 2030.Chini ya mpango huo, China inalenga kuweka nishati mpya ya umeme wa kilowati zaidi ya bilioni 2.8 kwenye gridi ya umeme na kujenga mtandao wa miundombinu ya kuchaji unaoweza kuunga mkono magari yanayotumia umeme zaidi ya milioni 110 ifikapo mwaka 2030.
Ili kufikia malengo hayo, mpango huo umeeleza kwa ufupi mambo mbalimbali yanayopewa vipaumbele, yakiwa ni pamoja na kupanua utoaji wa umeme wa kijani na wenye kutoa kaboni chache, kujenga gridi ya umeme iliyoratibiwa na himilivu zaidi, kuongeza unyumbulifu wa mfumo wa umeme, kuboresha usalama wa utoaji wa umeme, kusukuma mbele mageuzi ya sekta ya umeme yanayolenga soko, na kuhimiza ushirikiano wa kimataifa.
Mpango huo unatoa matakwa ya kujumuisha gridi ya kitaifa wakati wa kuendeleza nishati mbadala na kusukuma mbele miradi ya kawaida ya kuzalisha umeme kwa nishati ya maji kwa njia ya kisayansi, kuhimiza kazi ya kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia iendelezwe kwa usalama na utaratibu, kuhamasisha maendeleo mbalimbali ya kuzalisha umeme kwa nishati zisizo za visukuku, na kuongeza ufanisi na matokeo ya kaboni ya kuzalisha umeme unaotumia makaa ya mawe.
Kufikia mwaka 2030, China inapanga kuongeza uwezo wa mashine za uzalishaji wa umeme wa kawaida kwa nishati ya maji hadi kilowati takriban milioni 410, uwezo wa uzalishaji wa umeme kwa nishati ya nyuklia hadi kilowati takriban milioni 110, na uwezo wa pamoja wa mashine za uzalishaji umeme kwa nishati ya mabaki ya viumbe, nishati za joto la jua, jotoardhi na nishati ya bahari hadi kilowati takriban milioni 65.
China imeahidi kufikia kilele cha utoaji wa kaboni dioksidi kabla ya mwaka 2030 na kufikia msawazisho wa kaboni kabla ya mwaka 2060.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



