IRGC ya Iran yakataa madai ya Trump ya mazungumzo ya nyuma ya pazia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 18, 2026

Watu wakihudhuria hafla ya mazishi ya kamanda wa IRGC, ambaye aliuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel, Tehran, Iran, Aprili 1, 2026. (Xinhua/Sha Dati)

Watu wakihudhuria hafla ya mazishi ya kamanda wa IRGC, ambaye aliuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel, Tehran, Iran, Aprili 1, 2026. (Xinhua/Sha Dati)

TEHRAN - Kikosi cha Walinzi cha Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) kimekataa madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba kuna njia ya nyuma ya pazia ya mazungumzo kati ya Washington na IRGC.

Katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim linalomilikiwa kwa sehemu na serikali ya Iran jana Jumatatu, msemaji wa IRGC Hossein Mohebbi ameyaelezea madai hayo ya Trump kuwa "udanganyifu," akisema hakuna mazungumzo yanayoendelea kati ya maafisa wa IRGC na Wamarekani.

Hata vyombo vya kidiplomasia vya Iran kwa sasa havizungumzi na Marekani kutokana na "uvunjaji wa ahadi" wa Washington, Mohebbi ameongeza.

Kwa wakati tofauti, kwenye mkutano na waandishi wa habari wa siku hiyo ya Jumatatu, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amekanusha ripoti za vyombo vya habari kuhusu mawasiliano yasiyo rasmi kati ya Washington na IRGC kupitia maafisa wa Kundi la Kurdistan la Iraqi na mkutano unaodaiwa kuwa wa siri kati ya Marekani na Iran huko Erbil.

Habari hizo ni "mbinu za vyombo vya habari na operesheni za kisaikolojia zinazotumika kupanda mzozo miongoni mwa vyombo vya maamuzi vya Iran," Baghaei amesema.

Chombo cha Marekani cha Fox News kiliripoti mapema kwamba Trump amethibitisha kuwa kuna njia ya nyuma ya pazia ya mazungumzo ya amani kati ya Washington na IRGC.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha