Mkutano wa viongozi wa SADC wafunguliwa Durban, Afrika Kusini kwa wito wa mafungamano ya kina zaidi ya kikanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 18, 2026

DURBAN, Afrika Kusini – Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umefunguliwa jana Jumatatu katika mji wa Durban, Afrika Kusini kwa wito wa mafungamano ya kina zaidi ya kikanda na ushirikiano imara zaidi ili kusukuma mbele mageuzi ya kiviwanda na maendeleo ya kiuchumi.

Mkutano huo unafanyika chini ya kauli mbiu ya "Mageuzi ya kiviwanda yaliyo himilivu, endelevu na jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mabadiliko ya Kilimo na Madini Muhimu katika Kutafuta Dunia ya Haki."

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi amesema jumuiya hiyo ya kikanda inafanya kazi kuhimiza amani na usalama, kupanua biashara na uwekezaji, kuimarisha muunganisho wa miundombinu na kuongeza kina cha mafungamano ya kikanda.

Ametoa wito wa kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayowezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya kiuchumi na amehimiza nchi wanachama kukabiliana na changamoto za kikanda kupitia ushirikiano wa karibu zaidi.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesisitiza mafungamano ya kina zaidi ya kikanda ili kufungua uwezo wa kiuchumi na kuboresha maisha ya watu.

"Kanda hii ilirekodi ukuaji wa kiuchumi wa takriban asilimia 3.4 mwaka 2025, wakati huohuo biashara ya ndani ya SADC ilichukua takriban moja ya tano ya biashara yote," Ramaphosa amesema, akibainisha kuwa kanda hiyo bado haijatumia uwezo kamili wa soko lake lililofungamanishwa.

Ametoa wito wa juhudi kubwa zaidi za kusukuma mbele mageuzi ya kiviwanda na kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, vilevile kuongeza uwekezaji mkubwa zaidi katika miundombinu, ikiwemo barabara na reli zinazounganisha nchi wanachama na bandari za kisasa zinazounganisha Afrika ya Kusini na soko la barani na duniani.

Akibainisha kuwa jumuiya hiyo ya kikanda inapaswa kuwa jukwaa la kuwezesha wafanyabiashara kufikia soko pana zaidi la Afrika lenye watu zaidi ya bilioni 1.4, amesema: "Hii inahitaji tuondoe vizuizi visivyo vya ushuru, kuboresha usimamizi wa mipaka, kuoanisha viwango na kurahisisha mzunguko wa bidhaa, huduma, mitaji na ujuzi katika eneo letu."

Kwenye mkutano huo, Ramaphosa pia alichukua nafasi ya Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ya kuwa mwenyekiti wa zamu wa SADC.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha