Deni la taifa la Marekani lazidi dola trilioni 40 kwa mara ya kwanza katika historia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 20, 2026

Picha hii iliyopigwa Agosti 19, 2026 ikionyesha deni la taifa la Marekani likizidi dola trilioni 40 za Marekani, New York, Marekani. (Xinhua/Zhang Fengguo)

Picha hii iliyopigwa Agosti 19, 2026 ikionyesha deni la taifa la Marekani likizidi dola trilioni 40 za Marekani, New York, Marekani. (Xinhua/Zhang Fengguo)

WASHINGTON - Deni la taifa la Marekani limezidi dola trilioni 40 kwa mara ya kwanza katika historia, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani jana Jumatano.

Takwimu hizo zinaonyesha kwamba deni linaloshikiliwa na umma na lile linaloshikiliwa ndani ya serikali yalikuwa yamefikia dola trilioni 32.266 na dola trilioni 7.782, mtawalia, na kufanya jumla ya deni la umma kuwa dola trilioni 40.047 kufikia Jumanne wiki hii.

Hatua hiyo, iliyofikiwa miezi kadhaa mapema kuliko ilivyotarajiwa, inaonyesha nakisi isiyoisha ya bajeti ya serikali kuu ya Marekani, kwani matumizi yanaendelea kuzidi mapato, hali ambayo inaongeza deni la taifa.

Ripoti ya mwezi kutoka Wizara ya Fedha ya Marekani inaonyesha kwamba serikali kuu ilirekodi nakisi ya bajeti ya dola trilioni 1.367 katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2026, ambao ulianza Oktoba 1, 2025.

Deni la serikali kuu ya Marekani lilizidi dola trilioni 30 Januari 2022, likazidi dola trilioni 39 Machi 2026, na kufikia dola trilioni 39.7 Julai 2026.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimelielezea deni hilo la taifa kuzidi dola trilioni 40 kuwa ni hatua ya kutia hofu na mashaka kwa uchumi unaotegemea msingi wa fedha unaozidi kutetereka

"Ni dhahiri kuwa mwelekeo wetu wa sasa wa bajeti si endelevu," amesema Margaret Spellings, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sera cha Vyama Viwili vya Kisiasa. "Hata katika hali bora zaidi, tunaelekea kwa kasi kwenye jabali na tunakataa kugeuza gurudumu."

"Deni la serikali kuu tayari linaongeza gharama za maisha na kukandamiza matumizi na uwekezaji mwingine, likitishia uchumi wetu na ustawi wa muda mrefu wa Wamarekani," ameongeza.

Katika taarifa yake akijibu hatua hiyo yenye kutia wasiwasi, msemaji wa Ikulu ya White House Kush Desai amesema Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kusafisha usimamizi mbaya wa bajeti wa Rais wa zamani Joe Biden.

"Ndiyo maana utawala wa Trump umejikita katika kupunguza upotevu, ulaghai, na matumizi mabaya ya fedha za serikali kuu wakati huohuo umeharakisha ukuaji wa uchumi ili kurudisha uwiano wa deni la Marekani kwa Pato la Taifa kuelekea katika mwelekeo sahihi tena." Amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha