Lugha Nyingine
Wang Yi ahimiza maendeleo makubwa zaidi katika uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Korea Kusini

Rais wa Korea Kusini Lee Jae Myung akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Cheong Wa Dae, Seoul, Korea Kusini, Agosti 20, 2026. (Xinhua)
SEOUL - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kwamba anatumai Korea Kusini itafuata kithabiti sera ya kirafiki kuhusu China na kuchukua maadhimisho ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili mwaka ujao kama fursa ya kupata maendeleo makubwa zaidi katika uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Korea Kusini.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ameyasema hayo jana Alhamisi wakati alipokutana na Rais wa Korea Kusini Lee Jae Myung mjini Seoul.
“Kama nguvu muhimu kwa ajili ya kudumisha amani duniani, China siku zote inatetea utatuzi wa kisiasa wa migogoro ya kimataifa na kikanda kupitia mazungumzo,” Wang amesema, akiongeza kuwa China pia ni nguvu kubwa ya kuleta utulivu, ikitoa uhakika wenye thamani kwa dunia.
Wang pia amebainisha kuwa China iko tayari kunufaika na fursa za maendeleo pamoja na nchi zote, hasa majirani zake.
Katikati ya kukua kwa mafarakano ya uchumi duniani na kuongezeka kwa kujihami kibiashara, Wang amesema kuwa China na Korea Kusini zinapaswa kutoa mfano kwa kuhitimisha kipindi cha pili cha mazungumzo cha Mkataba wa Biashara Huria (FTA) mapema ili kuhimiza mafungamano ya kiuchumi ya kikanda na utandawazi wa kiuchumi ulio na manufaa na jumuishi kwa wote.
Kwa upande wake, rais huyo wa Korea Kusini amesema kwamba amefurahi kuona uhusiano kati ya China na Korea Kusini ukiboreka na kuendelea kwa haraka, huku ukiwa na kasi kubwa ya ukuaji katika ushirikiano wa kiuchumi na biashara.
Katikati ya hali ya sasa ya kimataifa, Lee amesema kwamba ushirikiano imara zaidi wa kimkakati kati ya Korea Kusini na China unatumikia maslahi ya msingi ya nchi zote mbili na ni muhimu kwa amani na utulivu wa kikanda.
“Korea Kusini na China zinapaswa kuwa washirika wanaotegemeana na wa kunufaishana wenye nguvu zinazokamilishana,” Lee amesema, akiongeza kuwa nchi hizo mbili zinahitajiana katika sekta kama vile uchumi, biashara na usalama.
Lee amesema anatazamia kufanya ziara katika Mji wa Shenzhen nchini China Novemba kwa ajili ya Mkutano wa Viongozi wa Uchumi wa APEC 2026, akiita ziara hiyo kuwa ni fursa muhimu ya kufanya kazi na China ili kusukuma mbele uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Korea Kusini na China hadi ngazi mpya.
Wakati wa ziara hiyo, Wang pia alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini Cho Hyun na Wi Sung-lac, mshauri mkuu wa usalama wa taifa wa rais wa Korea Kusini.

Rais wa Korea Kusini Lee Jae Myung akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Cheong Wa Dae, Seoul, Korea Kusini, Agosti 20, 2026. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



