Afrika Kusini yarudisha mabaki ya mababu kwa Namibia kwa ajili ya kurekebisha na kuponya majeraha ya kikoloni

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 21, 2026

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Gayton McKenzie (Kulia) akizungumza kwenye hafla ya kurejeshwa nyumbani katika Jumba la Makumbusho la Iziko la Afrika Kusini, Cape Town, Afrika Kusini, Agosti 19, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)

CAPE TOWN - Afrika Kusini imerudisha mabaki ya miili ya mababu na mabaki ya miili ya wafungwa wawili wa kisiasa wa Namibia kwenye hafla rasmi ya heshima ya kurudisha mabaki hayo iliyofanyika Jumatano wiki hii mjini Cape Town, mji mkuu wa utungaji sheria wa nchi hiyo.

Vyumba viwili vilijaa majeneza ya rangi ya pembe za ndovu, moja baada ya nyingine, kila moja likiwa limefunikwa kwa bendera ya Namibia. Mabaki hayo ya miili ya watu 84 wa jamii ya kiasili yalikuwa yamehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Iziko la Afrika Kusini kwa zaidi ya miaka 100 na imesemwa kuwa yalikuwa yakitumika kwa "sababu za kisayansi."

Mwenyekiti wa Baraza la Jumba la Makumbusho la Iziko la Afrika Kusini Marvin Mdhluli amesema: "Waliingia katika Jumba la Makumbusho la Afrika Kusini kama vitu vya utafiti wa sayansi bandia wenye msingi wa rangi," kwa lengo la kuonyesha watu wa jamii za kiasili kuwa ni wenye sifa na hadhi duni.

Kwenye chumba kingine kulikuwa na majeneza mawili yenye mabaki ya miili ya wafungwa wa kisiasa Festus Nehale, aliyefariki mwaka 1971, na Simon Petrus Nileng, aliyefariki mwaka 1974. Wote wawili walikuwa wamefungwa gerezani katika Kisiwa cha Robben, gereza maarufu la Afrika Kusini ambapo wafungwa wa kupinga ubaguzi wa rangi na wengine wa kisiasa walifungwa wakati wa ubaguzi wa rangi. Walizikwa Cape Town.

Wajumbe wa Namibia waliinamisha vichwa vyao kwa heshima mbele ya majeneza kabla ya kuhutubia wageni katika hafla hiyo.

Makabidhiano hayo pia yalijumuisha vitu vya kuzikwa na miili na sanamu za miili (body casts), ikiwa ni pamoja na shanga, mayai ya mbuni na vito vya mapambo kutoka Namibia.

"Kwa miaka mingi sana, mabaki ya wapigania uhuru wetu na mababu zetu yalitunzwa mbali na nchi waliyoiita nyumbani. Hii haikuwa haki kwao, familia zao na jamii zao," Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Gayton McKenzie amesema katika taarifa.

"Kwa kuwaleta mashujaa hawa wa kisiasa na mababu nyumbani, wakiwakilisha watu wa Makabila ya Waovambo, Wahimba, Wasan, Wanama, Wadamara na Waherero, tunarejesha heshima, utambulisho na nafasi yao halali katika nchi yao," amesema.

Waziri wa Elimu, Uvumbuzi, Vijana, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Namibia Sanet Steenkamp amesema mashujaa hao wa ukombozi watazikwa upya katika Makaburi ya Mashujaa ya Namibia Agosti 24.

"Sasa wanarudi kwa Namibia huru na yenye mamlaka," amesema. "Baadhi ya mababu hawa walichukuliwa kutoka kwa jamii zao na kuwa sehemu ya mkusanyiko wa sayansi ya kikoloni na makumbusho ya kikoloni ambapo walichukuliwa kuwa ni vitu, badala ya watu."

Majeneza yenye mabaki ya miili ya mababu wa Namibia yakionekana kwenye hafla ya kurejeshwa nyumbani katika Jumba la Makumbusho la Iziko la Afrika Kusini, Cape Town, Afrika Kusini, Agosti 19, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)

Waziri wa Elimu, Uvumbuzi, Vijana, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Namibia Sanet Steenkamp (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kurejeshwa nyumbani katika Jumba la Makumbusho la Iziko la Afrika Kusini, Cape Town, Afrika Kusini, Agosti 19, 2026. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha