Lugha Nyingine
Rais wa Iran asema Iran iko katika vita “vya pande zote" vya kiuchumi, kijeshi, na usalama

Picha hii ya faili ikimuonyesha Rais wa Iran Masoud Pezeshkian (kushoto) akizungumza wakati wa ziara yake kwenye makao makuu ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran (IRCS), Tehran, Iran, Aprili 15, 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema kwamba nchi hiyo iko katika vita “vya pande zote” vya kiuchumi, kijeshi, na usalama na "maadui."
Licha ya shinikizo hilo la Marekani, "tunasimama na kufanya juhudi za kuhudumia watu katika kukabiliana na vita hivi visivyo vya usawa," Pezeshkian amesema jana Jumapili katika hotuba kwa njia ya televisheni iliyorushwa na shirika rasmi la habari la Iran, IRNA.
Ameongeza kuwa serikali inafanya juhudi "za moyo wote" kupunguza mfumuko wa bei na kutatua matatizo ya kiuchumi ya watu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi akihudhuria sherehe ambapo Wizara za Mambo ya Nje na ile ya Afya za Iran zinasaini nyaraka ya makubaliano (MoU) juu ya ushirikiano katika kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa wakati wa vita, Tehran, Iran, Agosti 11, 2026. (Xinhua/Shadati)
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi amesema katika taarifa ya Jumapili kwamba Marekani haina njia nyingine ila kuzungumza kwa heshima na watu wa Iran, shirika hilo la habari, IRNA limeripoti.
Operesheni ya kiuchumi dhidi ya Iran inayodaiwa na Rais wa Marekani Donald Trump ni "hali inayojirudia na umwamba uleule ambao hutokea kila mara katika sera za Marekani," Araghchi amesema, akiongeza, "Kwa maana fulani, ni filamu inayojirudia ambayo tumeitazama mara kwa mara na tunajua namna ya kukabiliana nayo."
Katika ujumbe wake wa Jumatano wiki iliyopita kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alitangaza "operesheni ya kiuchumi ya kuharibu zaidi kuwahi kufanywa" dhidi ya nchi yoyote inayotoa njia ya uhai kwa Iran.
"Hii itakuwa Vita vya Kiuchumi na Kutengwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea," alisema, akiita hatua hiyo "SIKU INAYOWADIA YA KIUCHUMI."
Juni 18, Marekani na Iran zilisaini nyaraka ya makubaliano (MoU) juu ya kumaliza vita kwenye eneo hilo katika pande zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon. Chini ya MoU hiyo, zilikuwa zimepangwa kufanya mazungumzo ndani ya siku 60, ambazo zilimalizika Jumatatu wiki iliyopita, ili kufikia makubaliano ya mwisho, lakini hatma ya mazungumzo bado haiko dhahiri kufuatia kupamba moto kwa mivutano kati ya nchi hizo mbili mwezi uliopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



