Lugha Nyingine
Kenya yakamata washukiwa wanne katika kesi ya mauaji ya tembo
Watu wanne wamekamatwa kufuatia vifo vya tembo 18 katika hifadhi ya Amboseli nchini Kenya, huku mamlaka husika zikiendelea kutafuta washukiwa wengine.
Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya Rebecca Miano, amesema katika taarifa iliyotolewa Jumamosi kwamba vifo 15 kati ya hivyo vilirekodiwa kati ya Juni 24 na Julai 24, wakati vitatu zaidi viliripotiwa wiki iliyopita.
Miano amesema uchunguzi unaoendelea bado haujathibitisha hatia ya jinai, na kwamba serikali itaruhusu michakato ya uchunguzi na mahakama kuchukua mkondo wake na kushtaki yeyote atakayepatikana na hatia ya kuua, kuwapa sumu au kuwadhuru wanyamapori kinyume cha sheria.
Amesema kuwa Mamlaka ya Wanyamapori ya Kenya (KWS), kwa kushirikiana na mashirika ya usalama, upelelezi na ya kisayansi, imeimarisha uchunguzi kuhusiana na vifo hivyo, akibainisha kuwa uchunguzi wa kina kwenye eneo la tukio, uchambuzi wa kimaabara na uchukuaji wa sampuli za mazingira tayari vimeshafanyika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



