Lugha Nyingine
Iran yasema haitaacha vita viishe kulingana na masharti ya pande za "wachokozi"

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Agosti 24, 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema kwamba nchi yake haitaacha vita viishe kulingana na masharti yaliyowekwa na pande za "wachokozi".
"Hakika hatujawa upande wa kuanzisha hivi vita, lakini hatutaacha mwisho wa vita utegemee masharti ya pande za wachokozi," Baghaei ameuambia mkutano wa wiki na waandishi wa habari jana Jumatatu mjini Tehran.
Amesema kwamba Iran inaendelea kuazimia kulinda eneo lake na "haitalegeza msimamo na pande za wachokozi" au kujisalimisha kwenye "madai yao yaliyopitiliza."
Baghaei amepuuza madai ya Marekani kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz umefunguliwa na kwamba mamilioni ya mapipa ya mafuta yalikuwa yakipita humo kila siku, akiyaelezea kuwa ni sehemu ya "vita vya kisaikolojia na vya vyombo vya habari."
Pia amelaani operesheni mpya ya kiuchumi iliyotangazwa na Washington dhidi ya Iran, akisema Tehran itatumia "uwezo wake wote wa pande nyingi" kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani, ambavyo amevielezea kuwa ni pigo kwa biashara huria na mamlaka ya kitaifa.
Msemaji huyo pia ameonya kwamba nchi zinazosaidia operesheni za Marekani dhidi ya Iran zinaweza kukabiliwa na matokeo mabaya, na amekiita kizuizi cha majini cha Marekani kuwa ni "kitendo cha uchokozi."
Alipoulizwa kuhusu ripoti za vyombo vya habari vya Magharibi kwamba Iran inaweza kulenga kambi za Marekani barani Ulaya kama vita vitaanza tena, Baghaei amesema Iran ina haki ya kulenga chimbuko na chanzo cha "kitendo chochote cha uchokozi" kama nchi nyingine itaruhusu kambi, vituo na vifaa vyake kutumika kwa vitendo hivyo.
Israel na Marekani zilianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine ya Iran Februari 28, na kuwaua Kiongozi Mkuu wa wakati huo Ali Khamenei, makamanda wa kijeshi na raia. Iran ilijibu kwa mfululizo wa mashambulizi ya makombora na droni yaliyolenga Israel na kambi na mali za Marekani katika eneo hilo, na kuimarisha udhibiti wake kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, na kuzuia upitaji wa meli zinazomilikiwa au zinazohusiana na Israel na Marekani.
Usimamishaji mapigano ulifikiwa kati ya pande zinazopigana Aprili 8. Juni 18, Iran na Marekani zilisaini nyaraka ya makubaliano juu ya kumaliza vita katika pande zote, ikiwa ni pamoja na Lebanon.
Rais wa Marekani Donald Trump Jumatano wiki iliyopita alitangaza "operesheni ya kiuchumi ya kuharibu zaidi kuwahi kufanywa" dhidi ya nchi yoyote inayotoa njia ya uhai kwa Iran, akiita hatua hiyo "D-DAY YA KIUCHUMI."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



