Lugha Nyingine
Viongozi wa WHO na AU watoa wito wa mamlaka ya afya inayoongozwa na Afrika na kujitegemea

Wageni wakihudhuria Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 25, 2026. (Xinhua)
ADDIS ABABA -Viongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Afrika (AU) kwenye Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika Jumanne wiki hii wametoa wito wa mamlaka ya kujitegemea ya afya inayoongozwa na Afrika ili kumaliza utegemezi wa kihistoria wa bara hilo kwa ufadhili kutoka nje.
Mkutano huo unawaleta pamoja mawaziri wa afya wa Afrika na viongozi wa taasisi za afya za kikanda na kimataifa mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.
Mohamed Yakub Janabi, mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, amesema mkutano huo utafanya mapitio ya azma ya Afrika ya kujenga mustakabali wake wa afya na kutoa maamuzi na mapendekezo ya kuboresha huduma za afya katika bara zima.
"Hii ni hatua muhimu kuelekea kupunguza dola za kimarekani takriban bilioni 7 ambazo bara letu hutumia kila mwaka kuwapa rufaa wagonjwa nje ya nchi. Dira yetu ni rahisi: kuimarisha vituo vya ubora vya Afrika, kuunganisha wagonjwa wa Afrika na utaalamu wa Afrika, na kuufanya uwekezaji wa Afrika ufanye kazi kwa Afrika," Janabi amesema.
Janabi alisema, nchi za Afrika zimeimarisha mifumo ya ufuatiliaji, kupanua ufikiaji wa huduma muhimu za afya, kusukuma mbele upatikanaji wa huduma ya afya kwa wote, kuboresha uwezo wa usimamizi, na kukabiliana na milipuko kwa kasi na kuaminika kunakozidi kuongezeka katika kipindi cha miaka iliyopita.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf amesema Afrika inajitahidi kuweka mazingira ya mamlaka ya kujitegemea ya afya kupitia uzalishaji wa chanjo na ugawaji wa bajeti zinazoongezeka kila mara ili kuimarisha uwezo wake wa pamoja wa kuzuia, kubaini na kupambana na matishio ya kiafya.
"Kutokuwepo kwa mamlaka ya kujitegemea ya afya katika bara letu si jambo la hiari tena. Tunahitaji kutafuta namna ya kutumia njia zote zinazowezekana kufikia kujitegemea, kutoka kwenye ufadhili hadi uzalishaji wa ndani na utafiti na uvumbuzi," Youssouf amesema.
Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amebainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanatoa shinikizo isiyo ya kawaida kwa jumuiya za Afrika, wakati huohuo migogoro inavuruga huduma muhimu za afya, inafanya watu walio katika mazingira dhaifu kukimbia makazi yao, na kusababisha misukosuko ya kibinadamu ya kuvuka mipaka.
"Changamoto hizi kubwa zinatoa fursa ya kihistoria kwa Afrika kuimarisha sauti yake ya pamoja, kuongeza kwa kina ushirikiano wa kikanda, na kuchukua umiliki kamili wa mfumokazi wake wa afya," Atske Selassie amesema.
Mkutano huo wa 76 wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika uliopangwa kuendelea hadi kesho Ijumaa, unatarajiwa kuidhinisha sera za afya, mikakati na mipango ya kikanda kuboresha matokeo ya afya barani Afrika.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf akizungumza kwenye Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 25, 2026.(Xinhua)

Waziri wa Afya wa Ethiopia Mekdes Daba akizungumza kwenye Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 25, 2026.(Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



