Lugha Nyingine
China na Zimbabwe zaahidi kuzidisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Amon Murwira (kulia) na Naibu Waziri wa Biashara wa China Zhang Li wakipiga picha ya pamoja, Harare, Zimbabwe, Agosti 26, 2026. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)
HARARE - China na Zimbabwe zimesisitiza azma zao katika kuzidisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili kwenye Mkutano wa 11 wa Kamisheni ya Pamoja juu ya Ushirikiano wa Kiuchumi, Kiufundi na Biashara katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.
Mkutano huo, uliofanyika Jumatano wiki hii na kuongozwa kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Amon Murwira na Naibu Waziri wa Biashara wa China Zhang Li, umetoa jukwaa la kubadili makubaliano yaliyopo ya pande mbili kuwa fursa halisia za kiuchumi, ikiwemo kuongezeka kwa biashara na uwekezaji, uongezaji thamani na kutoa ajira.
Pande zote mbili zimekubaliana kutekeleza kikamilifu hatua 10 za ushirikiano zilizoanzishwa kwenye Mkutano wa Viongozi wa Beijing wa 2024 wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, kupanua na kurahisisha zaidi biashara ya pande mbili, na kuharakisha mazungumzo juu ya makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi kwa Maendeleo ya Pamoja.
Pia zimekubaliana kuhamasisha kampuni zaidi za China kuwekeza na kufanya shughuli zao nchini Zimbabwe, kuiunga mkono Zimbabwe katika kupanua na kuboresha mnyororo wake wa viwanda vya madini, na kusukuma mbele uboreshaji wa viwanda.
Murwira amesema China na Zimbabwe zinafurahia urafiki wa muda mrefu wenye msingi wa kuheshimiana na ushirikiano wa kimkakati, akibainisha kuwa ushirikiano huo umetoa maendeleo kinara katika sekta muhimu za uchumi wa Zimbabwe, zikiwemo za uzalishaji wa nishati, tija ya kilimo, na miundombinu.
"Zimbabwe imedhamiria kupanua biashara, kuhimiza uwekezaji, na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi zetu mbili," Murwira amesema.
Pia amekaribisha utozaji ushuru-sifuri wa China kwa nchi 53 za Afrika, jambo ambalo linawakilisha fursa kubwa za kupanua mauzo ya nje ya nchi hiyo, kama ilivyoonyeshwa na usafirishaji wa shehena ya kwanza ya blueberry wa Zimbabwe kwenda China mwezi Julai.
Kwa upande wake, Zhang amepongeza biashara ya pande mbili inayozidi kupanuka na mauzo ya nje ya Zimbabwe kwa China yanayozidi kuongezeka, akibainisha kuwa Zimbabwe imekuwa mpokeaji mkubwa wa uwekezaji wa China barani Afrika.
“China iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Zimbabwe ili kubadili makubaliano yote kuwa vitendo halisi na kusukuma mbele kwa kasi tulivu maendeleo yenye sifa bora ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara wa pande mbili,” amesema Zhang.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



