Lugha Nyingine
Maporomoko ya udongo na mawe yasababisha vifo vya watu 16 na wengine 546 hawajajulikana walipo, juhudi za uokoaji zafanyika kwa haraka Xizang

Waokoaji wakifanya utafutaji na uokoaji kwenye sehemu iliyoathiriwa na maporomoko ya udongo na mawe katika Wilaya ya Gyirong ya Mkoa Unaojiendesha wa Xizang, kusini magharibi mwa China, Agosti 29, 2026. (Xinhua/Jigme Dorje)
GYIRONG, Xizang - Waokoaji wanashindana na wakati na hali ngumu wakitafuta manusura baada ya maporomoko makubwa ya udongo na mawe yaliyosababishwa na kuporomoka kwa miamba ya barafu na theluji nchini Nepal, na kuikumba sehemu ya forodha ya mpakani ya Gyirong katika Mkoa Unaojiendesha wa Xizang kusini magharibi mwa China.
Kwa mujibu wa mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na ofisi ya habari ya serikali ya mkoa huo jana Jumapili, maafa hayo yaliyotokea Agosti 26, yamesababisha vifo vya watu 16 na na wengine 546 hawajajulikana walipo hadi ilipokuwa imefikia saa 12 jioni Jumamosi.
Ingawa waokoaji wanakabiliwa na mazingira magumu ya sehemu iliyoko kweye mwinuko wa juu kutoka usawa wa bahari na bonde lenye miamba mirefu inayochongoka, na hali ya hewa inayobadilika kila mara, waokoaji hao wanaendelea kusonga mbele kuingia katika sehemu ya kiini cha maafa hayo, kuondoa hatari barabarani, kufanya utafutaji na uokoaji, kukagua sehemu zenye hatari, kunyunyuzia dawa kuua vijidudu na kuzuia maambukizi ya maradhi, vilevile kusafisha na kurejesha hali ya kawaida ya njia zilizoharibiwa.
Mazingira ya sehemu zilizo kiini cha kufanyiwa uokoaji ni yenye hali ngumu sana. Waokoaji wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba sehemu hiyo ilikuwa imefunikwa na udongo na mawe yaliyoporomoka, na pia kuna maji ya mito yanayotiririka kwa haraka.
Wamesema matope yalikuwa na kina cha mita moja katika baadhi ya sehemu, ya kutosha kuzamisha hadi nusu ya mwili wa mtu, na hata katika sehemu yenye kina kifupi, matope kwa ujumla yalikuwa juu ya usawa wa kifundo cha mguu. Picha za video zilionyesha kuwa jengo la Forodha ya Gyirong lilikuwa limebomoka hadi kubaki na fremu yake ya chuma tu.

Waokoaji wakifanya utafutaji na uokoaji kwenye sehemu zilizoathiriwa na maporomoko ya udongo na mawe katika Wilaya ya Gyirong ya Mkoa Unaojiendesha wa Xizang, kusini magharibi mwa China, Agosti 30, 2026. (Xinhua/Jigme Dorje)
Jumapili asubuhi, eneo la kijeshi la Xizang la Jeshi la Ukombozi wa Umma la China lilituma timu ya kuzuia maradhi kwenye sehemu iliyoathiriwa na maafa kufanya kazi ya kunyunyiza dawa za kuua vijidudu na usafi wa mazingira, kufanya upimaji wa ubora wa chakula na maji, kutoa chanjo za dharura, na kufanya raundi za kawaida za matibabu kwa watu waliojeruhiwa na wagonjwa.
Hadi sasa, watu 2,141 wameshiriki kwenye utafutaji na uokoaji, wakiwemo watu kutoka Jeshi la Ukombozi wa Umma la China, Jeshi la Polisi la China, na kampuni ya serikali kuu ya Anneng ya China. Na magari 269 ya uokoaji na seti 3,922 za zana na vifaa vya uokoaji pia vimepelekwa kwenye mstari wa mbele.

Wafanyakazi wakifanya kazi kwenye kituo cha kupashana habari na data katika Mji mdogo wa Gyirong, wa Mkoa Unaojiendesha wa Xizang, kusini magharibi mwa China, Agosti 29, 2026. (Xinhua/Jigme Dorje)
Kwenye mkutano na waandishi wa habari, serikali ya mkoa huo pia imetaja kuwa maporomoko hayo ya udondo na mawe yalisababishwa na kuporomoka kwa miamba ya barafu na theluji kutoka kwenye mlima mrefu wa barafu nchini Nepal.
Barafu kwenye Mlima Langtang Lirung nchini Nepal ilipasuka kwenye mwinuko wa mita takriban 5,200 juu ya usawa wa bahari, na kusababisha kuporomoka kwa nguvu kwa mito ya barafu na kusababisha maporomoko ya miamba ya barafu na theluji. Maporomoko hayo yalianguka kwa haraka kwenye mwinuko wa mita takriban 4,000, yakigonga mlima mteremko na kukawa kuwa maporomoko ya udongo na mawe, ambayo yalielekea mbele kwa kasi na kusomba sehemu zenye kilomita 22 hivi hatimaye kufika Forodha ya Gyirong iliyoko kwenye sehemu yenye mwinuko wa mita 1,800 juu ya usawa wa bahari.
Maafa hayo yameteketeza kila kitu kwenye sehemu yenye kilomita za mraba takriban 0.7, na kuharibu kabisa majengo 27 na miundombinu husika kwenye sehemu hiyo ya forodha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



