Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wafunguliwa (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 09, 2026
Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wafunguliwa
Khalilur Rahman, Rais wa mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), akizungumza kwenye kikao cha kufungua mkutano huo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Septemba 8, 2026. (Xinhua/Zhang Fengguo)

UMOJA WA MATAIFA – Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) umetangazwa kufunguliwa rasmi na Khalilur Rahman, rais mpya wa Baraza Kuu, jana Jumanne.

Kwenye hotuba yake katika kikao cha ufunguzi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Rahman amesema anachukua jukumu lake hilo katika wakati muhimu wa mabadiliko kwa Umoja wa Mataifa.

“Wakati huu ambapo chombo hiki cha dunia kikiingia katika muongo wake wa tisa, mafanikio mengi yanastahili kutambuliwa,” amesema, akibainisha kuwa, wakati huo huo, chombo hicho cha dunia kinakabiliwa na changamoto kubwa.

Amesema Umoja wa Mataifa mara nyingi umeshindwa kufikia matarajio yaliyowekwa juu yake. Amebainisha kwamba, migogoro inaendelea kusababisha mateso makubwa kwa binadamu, mafanikio ya maendeleo yanabaki kuwa dhaifu na yasiyo thabiti na athari za tabianchi zinazidi kuongezeka.

"Kwa pamoja, changamoto hizi zimeifanya hali ya kuaminiana katika mfumo wa pande nyingi iwe chini ya shinikizo kubwa. Pengo la kuaminiana linalozidi kuongezeka linapima imani katika taasisi za kimataifa na hatua za pamoja – pengo ambalo lazima tulizibe kwa kufanya kazi pamoja kupitia mazungumzo, ushirikiano uliofanywa upya na matokeo," amesema Rahman.

Amesema ahadi yake kuu kwa mkutano huo wa 81 ni kufanya kazi bila kuchoka ili kufufua kuaminiana katika shirika hilo, ambalo amesema mafanikio ya hatua za pamoja za nchi wanachama hatimaye yanalitegemea. Amesema, imani hiyo ndiyo moyo ulio nyuma ya kaulimbiu ya mkutano huo 81 wa mwaka huu: "Kurejesha Kuaminiana, Kusimamia Mageuzi: Umoja wa Mataifa wenye Matokeo kwa Wote."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika hotuba yake, amesema mfumo wa kutatua matatizo duniani ni muhimu zaidi kuliko hapo awali katika nyakati hizi zenye misukosuko.

"Tunakabiliwa na migogoro, migawanyiko na hatari ya kuongezeka kwa nyuklia; umaskini na ukosefu wa usawa usiokoma; machafuko ya tabianchi yanayozidi kuwa mabaya; teknolojia kama akili mnemba (AI) ambayo inatoa matumaini makubwa lakini pia hatari kubwa bila usimamizi bora na uwazi kuzunguka athari zake kimazingira; na upigaji hatua wa polepole katika Malengo ya Maendeleo Endelevu," amesema.

Amesema sheria za kimataifa na haki za binadamu, ambavyo ni msingi wa Umoja wa Mataifa, mara nyingi hupuuzwa bila hatua stahiki kuchukuliwa. Aidha, ameongeza kuwa, hali ya kutoaminiana na kutiliana shaka katika siasa za kijiografia inaendelea kuzuia masuluhisho bora yanayohitajika, na kumomonyoa imani ya watu katika uwezekano wa ushirikiano wa kimataifa.

Guterres ameelezea matumaini kwamba chini ya uongozi wa Rahman, UNGA, kupitia diplomasia, mazungumzo na kufanya kazi kwa ushirikiano, inaweza kujenga upya kuaminiana na imani njema ambavyo vinakosekana katika siasa za kijiografia za leo, na kuhakikisha watu wa dunia wanarithi mustakabali ulio bora, mzuri na wenye amani zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha