Lugha Nyingine
Mkutano wa Usafiri wa Anga wa Afrika watoa wito wa ushirikiano wa kina zaidi ili kuongeza muunganisho wa anga (4)
![]() |
| Mwoneshaji bidhaa akiwaelezea wanafunzi shughuli za shirika la ndege kwenye Mkutano na Maonyesho ya 10 ya Usafiri wa Anga ya Afrika jijini Nairobi, Kenya, tarehe 9 Septemba 2026. (Xinhua/Yang Guang) |
NAIROBI - Viongozi na watunga sera wa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika kwenye Mkutano na Maonesho ya 10 ya Usafiri wa Anga ya Afrika yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya Jumatano na jana Alhamisi wametoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa kina zaidi wa kikanda katika sekta ya usafiri wa anga wa kiraia na utekelezaji kwa haraka zaidi wa Soko la Pamoja la Usafiri wa Anga barani Afrika (SAATM) ili kuongeza muunganisho ndani ya bara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mkutano na maonyesho hayo yamewakutanisha wajumbe wapatao 2,500 kutoka nchi zaidi ya 100, wakiwemo wawakilishi kutoka mashirika 135 ya ndege na waendeshaji wa huduma ya usafiri wa anga.
Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi, Musalia Mudavadi, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Kenya, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuanzisha anga la pamoja ili kuchochea biashara, utalii, na uwekezaji chini ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA).
"Usafiri wa anga si tu njia ya usafirishaji. Ni kiwezeshi cha biashara, utalii, uwekezaji, huduma za afya, elimu, usaidizi wa kibinadamu na mabadilishano ya kitamaduni," amesema Mudavadi.
Amebainisha kuwa SAATM, mpango kinara chini ya Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika, bado ni njia madhubuti ya kuondoa vikwazo zuizi, kupanua mitandao ya njia za safari, kuchochea ushindani, na kupunguza gharama za usafiri katika bara zima.
AdeSewa Adeyemi, Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga wa Kiraia ya Afrika, amezihimiza mamlaka za usafiri wa anga wa kiraia kote barani humo kuharakisha uoanishaji wa kanuni na utambuzi wa pamoja wa viwango vya ubora wa usalama.
Adeyemi amesema kuwa kuondoa vizuizi vya ufikiaji wa soko na kuoanisha mifumo ya udhibiti ni muhimu sana katika kufanikisha maono ya SAATM kwa mashirika ya ndege ya bara hilo.
Abderahmane Berthe, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mashirika ya Ndege ya Afrika, amesema kuwa changamoto za kimuundo, ikiwemo kodi kubwa za mafuta, kuyumba kwa sarafu, na mikataba ya huduma za anga ya pande mbili yenye vizuizi, vinaendelea kuathiri sana uwezo wa mashirika ya ndege kupata faida na upanuzi wa shughuli zao kikanda.
Berthe amesisitiza kuwa ushirikiano wa kina zaidi kati ya serikali na wadau wa sekta hiyo unahitajika kwa haraka na dharura ili kujenga mfumo imara na wenye uwezo wa kuushinda wa usafiri wa anga barani Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




