Maafisa wa Kenya wapongeza sera ya ushuru-sifuri ya China, watazamia ushirikiano na ukuaji wa biashara zaidi katika CIIE

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 06, 2026

Picha iliyopigwa Novemba 5, 2026 ikionesha Banda la Kenya kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China mjini Shanghai, mashariki mwa China. (People’s Daily Online)

Picha iliyopigwa Novemba 5, 2026 ikionesha Banda la Kenya kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China mjini Shanghai, mashariki mwa China. (People’s Daily Online)

SHANGHAI, China – Maafisa wa Kenya wamepongeza sera ya China ya ushuru-sifuri kwa nchi za Afrika, wakirejelea ukuaji mkubwa wa mauzo ya nje kwa soko la China na wametoa wito wa ushirikiano wa kina zaidi wa kibiashara wanaposhiriki kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE) yanayofanyika Shanghai, China.

Akiongoza ujumbe wa wafanyabiashara na wauzaji bidhaa nje wapatao 40 wa Kenya, Eric Rutto, Rais wa Shirikisho la Biashara na Viwanda la Kenya (KNCCI), ameyaelezea maonesho hayo kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha biashara za Kenya na soko kubwa la China.

"China ni soko kubwa. Ni soko ambalo wanachama wetu wangependa kulichunguza. Ni soko la aina yake la bidhaa za Afrika," Rutto amesema kwenye mahojiano na People’s Daily Online jana Alhamisi, Novemba 5 ndani ya banda la Kenya.

Amesisitiza uwepo unaozidi kukua wa shirikisho hilo nchini China, akibainisha kwamba KNCCI imeanzisha ofisi ya kudumu ya uwakilishi huko Changsha, mkoa wa Hunan, China, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 60 ya shirikisho hilo. Kwa mujibu wake, ofisi hiyo imekusudiwa kurahisisha miunganisho ya biashara, kutangaza bidhaa za Kenya na kusaidia mauzo kuja China.

Akizungumzia sera ya ushuru-sifuri ya China, iliyoanza kutekelezwa Mei 1, 2026, Rutto amesema tayari inatoa manufaa na fursa za kutia moyo kwa wauzaji nje wa Kenya.

Amesema takwimu za awali za biashara zilizokusanywa na shirikisho hilo zinaonesha ongezeko la wastani wa asilimia 8 hadi 10 la biashara, ingawa amesisitiza kwamba muda zaidi wa tathmini unahitajika ili kubaini mchango kamili wa sera hiyo.

Ameitaja tasnia ya maua ya Kenya kama mfano wa manufaa hayo, akibainisha kuwa maua ya Kenya hapo awali yalitozwa ushuru wa forodha wa asilimia 4 ili kuingia soko la China.

"Kuondoa ushuru huo wa asilimia 4 kumeongeza faida ambayo wauzaji nje wanaweza kupata. Pia sera hiyo inatufanya tuwe washindani zaidi dhidi ya nchi nyingine za Asia ambazo ziko karibu zaidi na China kijiografia," ameelezea.

Mtazamo huo umeungwa mkono na Dennis Mwirigi Murithi, Mwenyekiti wa Wakala wa Kukuza na Kutangaza Bidhaa Nje wa Kenya, ambaye ameeleza kwamba mauzo ya jumla ya Kenya kwenda China yameongezeka kwa asilimia 73 tangu utekelezaji wa sera hiyo ya ushuru-sifuri.

Dennis Mwirigi Murithi (kulia), Mwenyekiti wa Wakala wa Kukuza na Kutangaza Bidhaa Nje wa Kenya, akizungumza na wateja ndani ya Banda la Kenya kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China mjini Shanghai, mashariki mwa China, Novemba 5, 2026. (People’s Daily Online)

Ameyataja mazao ya kahawa na parachichi kuwa aina zenye ongezeko kubwa zaidi la mauzo ya nje, huku mauzo ya nje ya kahawa kuja China yakiongezeka kwa asilimia 241 na yale ya parachichi kwa asilimia 86.

Licha ya ukuaji huo wa kuvutia, Murithi amesema Kenya lazima ishughulikie ukuaji usio na uwiano wa mauzo yake ya nje na kuelewa vyema mapendeleo ya wanunuzi wa China.

Ameeleza kwamba ujumbe wa Kenya utaitumia CIIE ya mwaka huu kuwasiliana na wanunuzi wa China, kufahamu mahitaji ya soko na kutambua fursa za kuongeza ushindani wa bidhaa za Kenya.

Zaidi ya kilimo, Murithi amesema Kenya pia inachunguza fursa katika nguo na utengenezaji bidhaa, kwa lengo la kupanua mauzo yake ya nje na uwepo wake wa viwanda katika soko la China.

"Tunataka kuelewa kama viwanda vyetu vya nguo na utengenezaji pia vina fursa katika soko hili," Murithi amesema.

Murithi amesisitiza kwamba uhusiano imara wa kibiashara unaweza kuleta manufaa na ukuaji unaokwenda mbali zaidi ya takwimu za biashara.

Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China yanafanyika kuanzia Novemba 5 hadi 10, 2026 mjini Shanghai, China.

Eric Rutto, Rais wa Shirikisho la Biashara na Viwanda la Kenya (KNCCI), akipiga picha ndani ya Banda la Kenya kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China mjini Shanghai, mashariki mwa China, Novemba 5, 2026. (People’s Daily Online)

Dennis Mwirigi Murithi (kushoto), Mwenyekiti wa Wakala wa Kukuza na Kutangaza Bidhaa Nje wa Kenya akizungumza na mteja ndani ya Banda la Kenya kwenye Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China mjini Shanghai, mashariki mwa China, Novemba 5, 2026. (People’s Daily Online)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Renato Lu)

Picha