Lugha Nyingine
Mexico yasisitiza nafasi muhimu ya APEC katikati ya mabadiliko ya uchumi na biashara duniani
MEXICO CITY - Katika mabadiliko ya uchumi na biashara duniani, jukwaa la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia na Pasifiki (APEC) linatumika kama eneo muhimu kwa ajili ya majadiliano na uratibu juu ya namna mataifa yanavyofanya biashara, kukua, kuwekeza na kuzalisha katika karne ya 21, amesema Waziri wa Uchumi wa Mexico, Marcelo Ebrard.
Akizungumza jana Alhamisi kwenye mkutano wa kila siku na waandishi wa habari wa Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, Ebrard amesisitiza umuhimu wa Mexico kushiriki kwenye jukwaa hilo, akibainisha kuwa nchi hiyo inashika nafasi ya 10 duniani kwa mauzo ya nje na nafasi ya 13 kwa uchumi mkubwa duniani.
“Mexico ilichaguliwa kwa kauli moja kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo mwaka 2028, jambo linaloakisi utambuzi mpana kimataifa wa nchi hiyo” amesema.
Kuanzia tarehe 17 hadi 19 Novemba, Rais Sheinbaum atakuwa katika mji wa Shenzhen wa China kuhudhuria Mkutano wa 33 wa Viongozi wa Uchumi wa APEC.
Kwa mujibu wa Ebrard, mkutano huo unalenga kubainisha njia za kupunguza mivutano, kufikia makubaliano, na kusonga kuelekea ustawi wa pamoja, licha ya ushindani na tofauti zilizopo katika sera za biashara.
APEC inajumuisha uchumi wa wajumbe 21 kutoka eneo la Asia na Pasifiki ikiwa na lengo la kuwezesha biashara na uwekezaji, na kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



