Lugha Nyingine
Muziki waunganisha tamaduni na kuzidisha urafiki kwenye tamasha la Kichina nchini Kenya

Wanamuziki kutoka China na Afrika wakipiga picha baada ya tamasha la“Sauti za Kengele ya Dhahabu, Mapatano Kando ya Njia ya Hariri” jijini Nairobi, Kenya, tarehe 14 Novemba, 2026. (Xinhua/Liu Jiaqi)
NAIROBI - Tamasha la muziki la Kichina lenye jina la “Sauti za Kengele ya Dhahabu, Mapatano Kando ya Njia ya Hariri” lililojumuisha muziki wa jadi na maonesho ya tamaduni mbalimbali limefanyika jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya Jumamosi jioni, likiipa hadhira burudani ya muziki ya dakika 70 iliyosherehekea urafiki kati ya China na Afrika.
Tamasha hilo, liliandaliwa na Shirikisho la Wadau wa Fasihi na Sanaa la Beijing na kutekelezwa na Kundi la Kampuni za Sanaa na Burudani la China. Liliwakutanisha wasanii wa China na Afrika kwenye Ukumbi wa Kitaifa wa Sanaa za Maonesho wa Kenya.
Maonesho kwenye tamasha hilo yalijumuisha aina mbalimbali za muziki, zikiwemo nyimbo bora za pop na kazi zinazochanganya muziki wa jadi wa Kichina na ala ya piano.
"Ni heshima kubwa kwangu kuja Kenya wakati huu na kutambulisha utamaduni wa China kwa hadhira ya wenyeji," amesema mwimbaji maarufu wa China, Wu Bixia, ambaye aliimba wimbo wa jadi kutoka mkoa wa Yunnan unaoitwa "The River Flows Clear."
Ma Xinming, Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Shirikisho la Wadau wa Fasihi na Sanaa la Beijing, amesema ziara hiyo ya barani Afrika inalenga kutambua na kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa katika "Mwaka wa Mawasiliano kati ya Watu wa China na Afrika".
"Kwa muziki, inajenga jukwaa la mazungumzo ya kugusana mioyo, kuhimiza mabadilishano ya kitamaduni, kuzidisha kuelewana kati ya watu wa China na Kenya, na kuimarisha msingi wa kati ya watu wa urafiki kati ya China na Afrika," amesema.
Tamasha hilo lilihitimishwa kwa kutumbuiza wimbo wa pamoja wa "Jambo Bwana," wimbo maarufu wa kukaribisha wageni katika ukanda wa Afrika Mashariki. Wakati wasanii wakiimba na kucheza, watazamaji waliungana nao kwa kuimba kwa sauti, na kufuatiwa na makofi ya shangwe kwa muda mrefu mwishoni mwa onesho hilo.
Ma amesema kuwa kundi hilo litaendelea na ziara yake ya Afrika nchini Ethiopia baada ya onesho hilo la Kenya. Ameeleza matumaini yake kuwa wasanii hao watatembelea nchi zingine nyingi za Afrika katika siku za baadaye, ili kuendeleza zaidi ubadilishanaji wa kitamaduni na kuelezeana simulizi za urafiki kati ya China na Afrika.

Mwanamuziki Mchina Zhang Qianyuan (mbele) akipiga ala ya suona kwenye tamasha la "Sauti za Kengele ya Dhahabu, Mapatano Kando ya Njia ya Hariri" jijini Nairobi, Kenya, tarehe 14 Novemba, 2026. (Xinhua/Liu Jiaqi)

Mwanamuziki Mchina Wu Bixia akiimba kwenye tamasha la "Sauti za Kengele ya Dhahabu, Mapatano Kando ya Njia ya Hariri" jijini Nairobi, Kenya, tarehe 14 Novemba, 2026. (Xinhua/Liu Jiaqi)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



