Hotuba Kuu ya Xi Jinping katika Mkutano wa Maofisa Watendaji Wakuu wa APEC

(CRI Online) Novemba 19, 2026

Rais wa China Xi Jinping akihutubia hafla ya ufunguzi ya Mkutano wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Uchumi ya Asia-Pasifiki (APEC) 2026 kwenye Kituo cha Mkutano wa Kimataifa cha Qianhai huko Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, China. (Xinhua/Li Tao)

Rais wa China Xi Jinping akihutubia hafla ya ufunguzi ya Mkutano wa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO) wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia-Pasifiki (APEC) 2026 kwenye Kituo cha Mkutano wa Kimataifa cha Qianhai huko Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, China. (Xinhua/Li Tao)

"Kusonga Mbele kwa Imani Imara, Kujenga Mustakabali Mzuri kwa Asia-Pasifiki."

—Hotuba Kuu katika Mkutano wa Maofisa Watendaji Wakuu wa APEC

(Novemba 18, 2026, Shenzhen)

Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China

Wageni waheshimiwa,

Mabibi na mabwana,

Ndugu Marafiki:

Habari za Asubuhi! Ninapenda kuwakaribisha wote viongozi wa sekta za viwanda na wafanyabiashara za Asia na Pasifiki! Ninayo furaha kukutana nanyi nyote hapa Shenzhen.

Shenzhen, kwenye mwambao wa Bahari ya Kusini ya China, inakumbatia upepo unaovuma na mawimbi ya bahari. Katika kipindi cha miaka 40 na zaidi, Shenzhen imekuwa kielelezo katika juhudi za China za mageuzi na ufunguaji mlango. Imepata mabadiliko makubwa ya kihistoria, kutoka mji mdogo wa mpakani hadi kuwa jiji kubwa la kimataifa, ikitengeneza muujiza katika historia ya maendeleo duniani. Kuna mambo mengi watu wanaweza kujifunza kutoka kwenye mafanikio ya Shenzhen.

Leo hii, tunajikuta katika dunia inayobadilika na yenye misukosuko. Ukuaji wa uchumi duniani unakosa msukumo, na vitendo vya upande mmoja na kujihami kibiashara vinaenea kwa kasi. Wakati huo huo, biashara duniani inaendelea kukua dhidi ya mwelekeo huo, na mafanikio mapya yanapatikana katika teknolojia zinazoibuka kwa kasi zaidi, na kuleta athari kubwa katika mazingira ya maendeleo duniani. Ni nini kinaendelea duniani? Je, nini tunapaswa kufanya kwenye eneo la Asia-Pasifiki? Kufungua milango au kuifunga, kufanya kazi pamoja au dhidi ya kila mmoja, kuendana na mabadiliko au kubaki na njia za zamani? Haya ni maswali ya nyakati zetu ambayo ni lazima tuyajibu.

Kama msemo wa kale wa Kichina unavyosema, mbinu zote zinapaswa kubadilika kuendana na nyakati ili ziweze kuendelea kufaa. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia-Pasifiki (APEC) iliyoanzishwa katikati ya wimbi la utandawazi wa kiuchumi, imewezesha eneo la Asia-Pasifiki kuongoza mwelekeo wa nyakati zetu. Mwaka huu, China inakuwa mwenyeji wa mkutano wa APEC kwa mara ya tatu. Tuko tayari kushirikiana na pande zote ili kusonga mbele kwa imani imara, kujenga kwa pamoja jumuiya ya Asia-Pasifiki, na kuleta ustawi kwa wote katika eneo letu.

-Ili kuleta ustawi kwa wote katika eneo la Asia na Pasifiki, tunapaswa kudumisha amani na utulivu.

Hakuwezi kuwa na ustawi bila usalama, na hakuna usalama bila utulivu. Kutokana na mazingira tulivu katika eneo letu katika miongo iliyopita, Asia-Pasifiki imedumisha ukuaji thabiti wa uchumi na kuwa injini muhimu inayochochea ukuaji wa uchumi duniani. Kadiri hali ya nje inavyozidi kuwa tete, ndivyo inavyozidi kuwa muhimu kwa sisi kushikilia utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, na kuhimiza dunia ya ncha nyingi yenye usawa na utaratibu, na utandawazi wa kiuchumi ambao ni jumuishi na unaonufaisha wote. Na ni muhimu zaidi kwetu kutatua tofauti kupitia mazungumzo na mashauriano, na kuzishinda changamoto kupitia mshikamano na ushirikiano. Hii ndiyo njia ya kuweka msingi imara kwa amani na utulivu wa kudumu katika eneo la Asia-Pasifiki.

-Ili kuleta ustawi kwa wote katika eneo la Asia-Pasifiki, lazima tujenge madaraja ya kufungua mlango na ushirikiano.

Historia inatueleza kwamba kufungua milango kunaleta maendeleo wakati kufunga milango kunasababisha kubaki nyuma. Lazima tulinde kwa uthabiti mfumo wa biashara wa pande nyingi unaozingatia sheria huku Shirika la Biashara Duniani (WTO) likiwa msingi wake, tuunge mkono biashara na uwekezaji huria na wazi, na kuiweka minyororo ya viwanda na ugavi duniani katika hali ya utulivu na uendeshaji usiokwamishwa. Tunapaswa kufanya kazi kwa kasi tulivu kuelekea Eneo la Biashara Huria la Asia-Pasifiki, tujenge mtandao wa pande nyingi wa muunganisho, tuongeze ushirikiano katika maeneo kama vile biashara ya kidijitali, biashara ya mtandaoni ya kuvuka mipaka, na forodha za kidigitali, na kuzidisha ushirikiano wa kimataifa katika minyororo ya viwanda na ugavi. Vyote hivi vitaandaa njia kwa ajili ya utandawazi wa kiuchumi wa Asia-Pasifiki.

-Ili kuleta ustawi wa pamoja katika eneo la Asia-Pasifiki, tunapaswa kuimarisha uvumbuzi ili kuchochea ukuaji.

Uvumbuzi ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii. Wanachama wa APEC wamechochea uvumbuzi wa sayansi na teknolojia duniani, kampuni mpya za teknolojia na modeli kubwa za AI zimeibuka kwa wingi, na uvumbuzi mwingi umewezesha maelfu ya sekta mbalimbali na kufikia kila kaya. Tunapaswa kujenga ushirikiano wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi, kuzidisha ushirikiano katika uchumi wa kidijitali na AI na kuhimiza mageuzi ya kijani na ya kutoa kaboni chache. Kwa kufanya hivi; tunaweza kubadilisha nguvu katika uvumbuzi kuwa vichocheo vya ukuaji, na kutoa msukumo mkubwa kwa ukuaji wa uchumi katika Asia-Pasifiki.

-Ili kuleta ustawi wa wote katika eneo la Asia-Pasifiki, tunapaswa kupanua njia za kusaidiana na kunufaishana na yenye matunda kwa pande zote.

Kwa kuwa nchi na maeneo mbalimbali ya uchumi katika eneo la Asia na Pasifiki yana tofauti katika historia, tamaduni, na hatua za maendeleo, kuchukua mbinu moja kwa wote hakuwezi kuendeleza ushirikiano. Tunapaswa kuondoa vizuizi vya biashara na uwekezaji ili kujenga uchumi ulio wazi wa Asia-Pasifiki. Wakati huohuo, tunapaswa kuhimiza maendeleo ambayo ni yenye uwiano na yenye kuleta manufaa kwa wote ili kuhakikisha usawa na ufanisi. Tunapaswa kufuata falsafa ya kuweka kipaumbele kwa maendeleo ya watu, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia na makundi ya uchumi unaoendelea, na kuzidisha ushirikiano katika usafirishaji, afya ya umma, nishati, usalama wa chakula, na kupambana na ufisadi na nyanja nyingine, ili kwamba matunda ya maendeleo yachangiwe na pande zote za kiuchumi, makundi na jamii zote.

Eneo la Asia-Pasifiki ni nyumbani kwa maeneo muhimu zaidi ya ghuba duniani, hasa kwa uchumi wake ulio wazi, ushirikiano, na wenye athari zinazoenea. Shenzhen, mahali tunapokutana sasa, ni sehemu ya Eneo Kuu la Ghuba ya Guangdong-Hong Kong-Macao. China inaunga mkono kuanzishwa kwa Shirikisho la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Maeneo ya Ghuba Duniani, kwa lengo la kuzidisha mawasiliano na maingiliano kati ya maeneo ya ghuba duniani. Hii itatusaidia kutafuta njia mpya za ushirikiano wa kiuchumi katika eneo la Asia na Pasifiki.

Waheshimiwa wageni na marafiki!

Mwaka huu ni mwanzo wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China. Uchumi wa China unadumisha kasi ya ukuaji wenye sifa bora unaochochewa na uvumbuzi, jambo linaloonesha uhimilivu mkubwa na uhai imara. Katika robo tatu za kwanza, ukuaji wa uchumi wa China ulifikia 4.6%. Nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora zinaendelea kwa kasi, muundo mpya wa maendeleo unajengwa kwa haraka, mabadiliko ya kijani na ya kutoa kaboni chache yanashika kasi. Mpango wa 15 wa Miaka Mitano umekuwa na mwanzo mzuri. Ukiwa ni mwongozo wa maendeleo ya China, Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China pia unatoa orodha ya fursa kwa ajili ya kuhimiza ukuaji wa uchumi katika eneo la Asia-Pasifiki na duniani. Kwa kweli, huu ni mwaliko wa ushirikiano ambao China imetuma kwa sekta ya viwanda na biashara katika sehemu mbalimbali duniani.

-China itaipa sekta za viwanda na biashara duniani soko kubwa zaidi na lililofungua mlango.

China ni soko la pili kwa ukubwa duniani la watumiaji, ina kundi kubwa zaidi la watu wa kipato cha kati duniani na ina uwezo mkubwa katika uwekezaji na matumizi. Kuanzia magari yanayotumia nishati mpya hadi nyumba zinazotumia mifumo janja, kuanzia uchumi wa wazee hadi utalii wa theluji na barafu, kila sekta mpya inatoa fursa mpya kwa kampuni kote duniani. China inapoharakisha maendeleo ya soko lililofungua mlango na kupanua uagizaji wa bidhaa na huduma zenye ubora wa juu, mahitaji mengi mapya yatajitokeza. Siku chache zilizopita, Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa Nje ya China yalifanyika Shanghai. Wengi wenu mlioko hapa leo mlihudhuria maonesho hayo na kupata fursa mpya za ushirikiano. China pia itaendelea kuandaa mfululizo wa shughuli za "Kuuza Bidhaa China," na nyinginezo ili kufungua njia bora za kusaidia bidhaa bora za nchi mbalimbali kuingia katika soko la China.

-China itaipa sekta ya viwanda na biashara duniani mazingira bora ya maendeleo.

Ukuaji unaoendeshwa na uvumbuzi na mabadiliko ya kijani ni maneno muhimu kwa uchumi wa China. Kuanzia roboti za viwandani na mashambani, hadi magari yanayojiendesha yenyewe na upelekaji bidhaa kwa droni, China ni uwanja mkubwa wa majaribio ya uvumbuzi ambako teknolojia mpya za kisasa zinapimwa na kuboreshwa katika mazingira halisi, na kisha baadaye kubadilishwa kuwa vichocheo vyenye ubora wa juu vya ukuaji. China itaharakisha ujenzi wa mfumo sanifu wa kiviwanda, kuhimiza mafungamano ya kina kati ya uvumbuzi wa kiteknolojia na viwanda. Itaunga mkono mageuzi na uboreshaji wa sekta za jadi, upanuzi wa sekta zinazoibuka, na mpangilio wa kutazama mbele wa sekta za siku za baadaye. Hii itatoa msukumo mkubwa kwa uvumbuzi wa teknolojia na ukuaji wa kampuni duniani.

-China itaipa sekta ya viwanda na biashara duniani mazingira ya ushirikiano unaoimarishana.

Mwaka 2001, China iliandaa Mkutano Usio Rasmi wa Viongozi wa APEC kwa mara ya kwanza na kujiunga na WTO katika mwaka huo huo. Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, China imetimiza kikamilifu ahadi zake kwa WTO. Wakati ikitafuta maendeleo yake yenyewe, China imetoa fursa kwa nchi nyingine na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya pamoja. China imekuwa ikipinga vitendo vya upande mmoja na kujihami kibiashara, na imetekeleza kwa mfumo wa kweli wa pande nyingi. Imekuwa ikishikilia kwa uthabiti mfumo wa biashara wa pande nyingi na kanuni za WTO, na kusukuma mbele mageuzi ya WTO, na imeleta utulivu na uhakika katika ukuaji wa uchumi wa dunia na ushirikiano wa kiuchumi na biashara wa kimataifa. Bila kujali hali ya kimataifa inavyobadilika, China haitabadilika katika kushirikiana na kufikia matokeo ya kunufaishana na nchi nyingine.

China inaendelea kudhamiria kithabiti kwa ushirikiano wa kiwango cha juu wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na inakaribisha ushiriki wa kampuni za eneo la Asia-Pasifiki ili tuweze kujenga fursa za ukuaji na kuchangia matunda ya maendeleo pamoja. China si tu itapunguza ushuru na kupanua ufikiaji wa soko lakini pia inachukua hatua zaidi—tutafanya mageuzi katika maeneo yenye changamoto kama vile kanuni, usimamizi, na vigezo ili kuhakikisha kikamilifu ufikiaji wa soko. Hii inajumuisha kutekeleza kikamilifu haki za upatikanaji wa soko na uendeshaji kwa sekta ya uzalishaji viwandani na kupanua ufunguaji wa sekta ya huduma kwa utulivu.

Waheshimiwa wageni na marafiki!

Asia-Pasifiki ni nyumbani kwetu. Ni hapa ambapo kwa pamoja tunatafuta maendeleo na ushirikiano. Jumuiya za wafanyabiashara katika eneo la Asia-Pasifiki ni wanaoongoza wa uchumi duniani. Natumai kwamba mtaendeleza moyo wa ujasiriamali, kufuata kithabiti uvumbuzi na ubora wa hali ya juu, kubaini na kupanua fursa kwa ajili ya ushirikiano wa kibiashara, na kuchangia zaidi katika kuhimiza mtangamano wa kiuchumi katika eneo la Asia-Pasifiki. Mnakaribishwa kuendelea kushiriki zaidi katika juhudi za China za kuleta mageuzi na ufunguaji mlango, na ujenzi wa mambo ya kisasa, pamoja na kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya kisasa ya China.

Hebu tushikane mikono kukabiliana na changamoto zinazokabili maendeleo kupitia ufunguaji mlango, kuongeza kasi ya ukuaji kupitia uvumbuzi, na kutafuta manufaa kwa wote kupitia kushirkiana. Hebu tufanye kazi pamoja kujenga jumuiya ya Asia-Pasifiki na kuleta mustakabali mwema kwa eneo letu!

Asanteni.

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Picha/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha