Lugha Nyingine
Chama tawala nchini Uganda chatafuta kuzidisha ubadilishanaji na ushirikiano na CPC

Picha hii iliyopigwa tarehe 17 Novemba, 2026, ikionesha mkutano na waandishi wa habari juu ya mkutano wa tano wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) mjini Kampala, Uganda. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA - Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM), Richard Todwong, amesema kuwa mkutano wa tano uliohitimishwa hivi karibuni wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) umetoa masomo ya thamani katika ujenzi na usimamizi wa Chama na kudumisha uhusiano wa karibu na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne wiki hii katika Ubalozi wa China nchini Uganda, Todwong amesema kuwa NRM inakiona Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kuwa mshirika muhimu wa kitaasisi na kimkakati, ambaye kutoka kwake ina mengi ya kujifunza na kuchangia.
"Somo moja muhimu ni kwamba vuguvugu la mapinduzi halipaswi kamwe kubweteka juu ya uimara wake wa kitaasisi. Ni lazima kila wakati kufanya upya miundo ya chama, kuimarisha mifumo yetu ya ndani, kuandaa viongozi wenye uwezo, na kudumisha uhusiano wa karibu na wananchi," amesema Todwong.
Amesema NRM ina matumaini ya kusukuma uhusiano wake na CPC kuelekea "ushirikiano uliopangwa vizuri zaidi, wa kivitendo, na wenye mwelekeo wa matokeo."
Amesema katika nyanja ya uchumi, NRM inashauku hasa katika kujenga majukwaa ya kuunganisha utaalamu wa maendeleo na fursa za uwekezaji za China na vipaumbele vya Uganda katika kilimo, utengenezaji bidhaa, maendeleo ya viwanda, nishati, na teknolojia.
"Tunashauku hasa kwenye uzoefu wa China katika maendeleo ya viwanda, kukifanya kilimo kuwa cha kisasa, usindikaji wa mazao ya kilimo, uhamishaji teknolojia, kupunguza umaskini, na kutengeneza utajiri," amesema Todwong, akiongeza kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa Uganda wakati inatekeleza ilani ya NRM ya mwaka 2026-2031 na kufuata malengo yake ya maendeleo ya kitaifa.
Kiongozi huyo pia ametoa wito wa mabadilishano ya kina zaidi katika nyanja za ujenzi wa chama, usimamizi wa taasisi, uwajibikaji na nidhamu ya uongozi, vilevile kupanua ushirikiano katika usimamizi wa chama kidijitali, usimamizi wa vyombo vya habari, na teknolojia za mawasiliano.
Balozi wa China nchini Uganda Wu Guangrong amewafahamisha waandishi wa habari juu ya mkutano huo wa tano wa wajumbe wote, uliofanyika Beijing kuanzia Oktoba 26 hadi 29. Wu amesema mkutano huo ulijikita katika Chama kujiendesha kwa nidhamu kali kwa pande zote.
Mjumbe huyo amepongeza ushirikiano kati ya NRM na CPC, akibainisha kuwa vyama vyote viwili vinathamini umoja wa kitaifa, kutafuta maendeleo yanayofaa kwa nchi zao na hutoa kipaumbele katika kuboresha maisha ya watu.
"Tuna mengi ya kujadili, ikiwemo namna ya kutoa mafunzo kwa maafisa wanaoelewa mahitaji ya ndani na namna ya kuweka sera za maendeleo katika vitendo. CPC kiko tayari kuzidisha mabadilishano haya na NRM katika moyo wa kuheshimiana, usawa na kufunzana," Wu amesema.

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China

Shughuli ya Siku ya Meli ya "Xuelong 2" ya China kufunguliwa kwa umma yafanyika Hainan
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma