Mkutano wa COP31 washindwa kufikia mwafaka juu ya Mkataba wa Antalya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2026
Mkutano wa COP31 washindwa kufikia mwafaka juu ya Mkataba wa Antalya
Picha hii iliyopigwa Novemba 22, 2026 ikionesha kikao cha kuhitimisha Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) mjini Antalya, Uturuki. (Xinhua/Liu Lei)

ANTALYA, Uturuki - Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) umeshindwa kufikia mwafaka juu ya Mkataba wa Antalya uliopendekezwa, Rais wa COP31, Murat Kurum, amesema jana Jumapili.

Kauli yake hiyo imetolewa kwenye kikao cha kuhitimisha mkutano huo, baada ya rasimu ya tatu kuwasilishwa mapema siku hiyo, siku karibu mbili baada ya muda uliopangwa wa kuhitimisha mkutano huo, ambao ulikuwa Ijumaa.

"Inaonekana kuna pande zinazopinga nyaraka hizi. Ninaelewa kuwa hakuna makubaliano juu ya nyaraka hizi. Kwa sababu hiyo, maamuzi haya hayajapitishwa," Kurum, ambaye pia ni Waziri wa Mazingira, Maendeleo ya Miji na Mabadiliko ya Tabianchi wa Uturuki, aliwaambia wajumbe.

"Nyaraka hizi hazikulazimishwa kwa yeyote," alisema, akibainisha kuwa uongozi wa mkutano huo ulikuwa umesikiliza matakwa ya nchi mbalimbali moja baada ya nyingine na kufanya kazi mchana na usiku ili kupunguza tofauti za mitazamo.

Mapema, wakati wa kuanza kwa kikao hicho, Kurum aliwasilisha rasimu hiyo kama matokeo ya michango ya pamoja ya wajumbe inayogusia masuala ya nishati ya umeme, lengo la kuweka kikomo cha ongezeko la joto duniani katika nyuzi joto 1.5 Selsiasi juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, fedha kwa ajili ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala ya bahari.

"Hakuna aliyepata kila kitu alichokitaka. Hata hivyo, kila mmoja anaweza kujiona katika nyaraka hizi. Maana ya mwafaka ndiyo hii pia," alisema, kabla ya mapingamizi kutoka kwa washiriki kuzuia kupitishwa kwa rasimu hiyo.

Mkutano huo wa COP31 ulifunguliwa rasmi Novemba 9 katika mji wa mapumziko wa Antalya, uliopo kando ya Bahari ya Mediterania kwa kujikita zaidi katika kubadilisha ahadi juu ya tabianchi duniani kuwa vitendo halisi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha