Lugha Nyingine
TAZARA katika miaka 50: reli ya zamani, mwanzo mpya

Picha hii iliyopigwa tarehe 13 Novemba 2026 ikionesha jukwaa la Stesheni ya New Kapiri Mposhi ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) huko Kapiri Mposhi, Jimbo la Kati, Zambia. (Xinhua/Liu Qiong)
LUSAKA - Johnny Kaela alikuwa miongoni mwa Wazambia wa kwanza kuajiriwa kujenga Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) mwaka 1971. Akiwa na umri wa miaka 76, anashuhudia wafanyakazi wakianza tena kufanya kazi kwenye reli hiyo.
"Kama inaweza kurejeshwa katika viwango tulivyokuwa navyo wakati ule," amesema, "itakuwa ni mafanikio makubwa."
Reli ya Tanzania-Zambia, inayojulikana kwa jina la TAZARA, ina urefu wa kilomita takriban 1,860 kutoka bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania hadi New Kapiri Mposhi nchini Zambia, nchi isiyo na bandari.
Reli hiyo iliyojengwa na China, Tanzania, na Zambia kati ya mwaka 1970 na 1976, mwaka huu inatimiza miaka 50. Mwaka mmoja uliopita, tarehe 20 Novemba 2025, nchi hizo tatu zilizindua mradi wa kuifufua reli hiyo, zikilenga kuongeza uwezo wake wa kusafirisha mizigo hadi mara kumi na mbili.
Wajenzi
"Kazi ilikuwa ngumu. Tulikuwa na mashine za zamani," amesema Kaela akikumbushia hali ya miaka ya 1970. Wazambia hawakuzungumza Kichina, na si wataalamu wote Wachina waliweza kuzungumza Kiingereza. "Lakini tuliweza kuelewana. Tuliweza kuwasiliana kwa ishara za mikono."
"Kama tungefuata mfumo wa kufanya kazi kwa saa nane kwa siku, mradi huu ungechukua miaka zaidi ya 10," amesema. "Lakini tulifanya kazi kwa zaidi ya saa 12 kwa siku."
Reli hiyo ilikamilika kabla ya muda uliopangwa. "Iliwezesha usafirishaji wa bidhaa kati ya hapa na Dar es Salaam. Iliboresha maisha ya watu na kutengeneza ajira," amesema Kaela, ambaye alipandishwa cheo na kuwa msimamizi wa kazi na kubaki kwenye reli hiyo hadi alipostaafu.
Wakarabati
Nje ya stesheni ya New Kapiri Mposhi, miti ya maua mekundu iliyopandwa wakati stesheni hiyo inajengwa imechanua kikamilifu. Wafanyakazi Wachina kwenye mradi huo wanaijua miti hiyo kwa jina lingine, mti wa phoenix, linalotokana na ndege dhahania anayefufuka kutoka kwenye majivu yake mwenyewe. Wana matumaini kuwa reli hiyo itafanya vivyo hivyo.
"Inamaanisha kukarabati njia iliyopo na kurejesha uwezo wake wa kubeba mizigo, si kujenga njia mpya," amesema Lin Wenzong, naibu meneja wa mradi huo katika sehemu ya Zambia anayefanya kazi katika Shirika la Uhandisi wa Ujenzi la China (CCECC) linayotekeleza mradi huo.
Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, wafanyakazi watakarabati reli kwenye njia nchini Zambia yenye urefu wa kilomita 884, pamoja na madaraja, stesheni, na msingi wa reli hiyo. Lin amesema kuwa baada ya kukamilika, reli hiyo inatarajiwa kusafirisha tani milioni 2.4 za mizigo kwa mwaka, ikilinganishwa na tani 200,000 zinazosafirishwa sasa. Aidha, muda wa safari utapungua hadi theluthi moja tu ya muda unaotumika sasa, huku gharama za usafirishaji zikiwa chini kwa asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na usafiri wa barabarani.
Mradi huo unaajiri wenyeji 500, idadi ambayo inatarajiwa kufikia zaidi ya 2,000 wakati wa kilele cha utekelezaji wa mradi huo. "Tunatumai kuwa wakati mradi utakapokamilika, utaacha wataalamu wa reli ambao wataendelea kufanya kazi hapa," amesema Lin.
Kizazi kijacho cha wahandisi
Baadhi ya wale waliopoteza maisha yao wakati wa ujenzi wa reli hiyo wamezikwa katika Bustani ya Kumbukumbu ya TAZARA, iliyoko nje kidogo ya Lusaka, mji mkuu wa Zambia. Uwanja wake wa kumbukumbu una umbo la pembetatu, ukiwa umebuniwa kwa kuiga kishuke cha maua matatu ya 'bougainvillea'.
"Maua haya matatu yanaungana na kuwa kitu kimoja, kama tu ilivyo kwa nchi hizi tatu," amesema Mundia Siyamana, mfanyakazi mwenyeji wa CCECC, ambaye pia ni mwongozaji wa watalii katika bustani hiyo. Bustani hiyo hutembelewa na watu hadi 200 kwa siku.

Mtembea kwa miguu akipita karibu na Stesheni ya New Kapiri Mposhi ya Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA) huko Kapiri Mposhi, Jimbo la Kati, Zambia, Novemba 13, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)

Watalii wakipiga picha kwenye Bustani ya Kumbukumbu ya TAZARA jijini Lusaka, Zambia, Novemba 14, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)

Picha hii iliyopigwa Novemba 14, 2026 ikionesha mandhari ya Bustani ya Kumbukumbu ya TAZARA jijini Lusaka, Zambia. (Xinhua/Liu Qiong)

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China

Shughuli ya Siku ya Meli ya "Xuelong 2" ya China kufunguliwa kwa umma yafanyika Hainan
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma