Lugha Nyingine
China yawa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika maombi ya hataza za 6G

Picha hii iliyopigwa Novemba 6, 2026, ikionesha mfano wa awali wa kifaa cha 6G cha Qualcomm, ambacho kilioneshwa kwa mara ya kwanza duniani kwenye Maonesho ya tisa ya Kimataifa ya Ugizaji Bidhaa Nje ya China (CIIE), mjini Shanghai, mashariki mwa China. (Xinhua/Cao Mengyao)
SHANGHAI - China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika maombi ya hataza za 6G na imetengeneza mali muhimu zaidi ya 300 za teknolojia ya 6G, kwa mujibu wa Mkutano wa Maendeleo ya 6G Duniani 2026 uliofanyika Shanghai jana Jumanne.
"Mitandao yetu ya 5G imekuwa ikifanya kazi kwa miaka mingi, ikiweka msingi imara kwa ajili ya mabadiliko kuelekea 6G, na msingi huu pia umenufaika kutoka kwenye ushirikiano katika tasnia hii duniani," amesema Wen Ku, mwenyekiti wa Jumuiya ya Viwango vya Mawasiliano ya China. Amesema, kufikia mwisho wa mwezi Agosti, China ilikuwa imejenga vituo vya msingi vya 5G takriban milioni 5.19.
"Kuanzia 3G hadi 5G, viwango vyenye mifumo sawa duniani vimeleta uchumi wa kiwango kikubwa na hivyo kupunguza sana gharama za vifaa vya mawasiliano na kuunganisha mabilioni ya watu na ulimwengu wa kidijitali; na 6G inapaswa kuendelea kwenye njia hiyo ya maendeleo ya ushirikiano.” Wen amesema.
Zhong Zhihong, mhandisi mkuu katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Kupashana Habari ya China, amesema teknolojia ya 6G kwa sasa iko katika hatua muhimu ya kuongeza mafanikio mapya ya kiteknolojia na kuendeleza uundaji wa vigezo vya pande zote, jambo ambalo linabainisha umuhimu zaidi wa wadau wa tasnia hiyo, wasomi, na pande za utafiti duniani kujenga maelewano na kushirikiana kwa karibu.
Kwenye mkutano huo, kundi la uhamasishaji la IMT-2030 (6G), pamoja na mashirika makubwa ya kimataifa, miungano ya tasnia hiyo, na kampuni ongozi za China na kimataifa, wametoa Tamko la Falsafa ya Maendeleo ya 6G Duniani
Tamko hilo linaainisha dhana tano, ikiwemo uvumbuzi jumuishi unaovuka nyanja mbalimbali ukiwa na uwezo wa ndani wa AI katika msingi wake; maendeleo endelevu na ya kijani katika mnyororo mzima wa thamani; pamoja na mfumo salama na wa kuaminika wenye msingi wa usalama katika nyanja zote, miongoni mwa mengine.
Mkutano huo pia umezindua mpango wa majaribio kwa ajili ya maendeleo ya uvumbuzi wa 6G, ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya wizara hiyo na serikali za mikoa. Maeneo manane ya ngazi ya mkoa ya China ambayo ni Beijing na Hebei kaskazini mwa China; Shanghai, Jiangsu, Zhejiang na Anhui mashariki mwa China; Hubei katikati mwa China; na Guangdong kusini mwa China yanashiriki katika kujenga kwa pamoja mfumokazi wa kitaifa ulioratibiwa kwa ajili ya uvumbuzi wa 6G.

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China

Shughuli ya Siku ya Meli ya "Xuelong 2" ya China kufunguliwa kwa umma yafanyika Hainan
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma