Lugha Nyingine
Vijana wa Afrika wahimizwa kuunda mustakabali wa bara hilo kwenye mkutano wa Kigali

Rais wa Rwanda Paul Kagame akitoa hotuba yake kwenye hafla ya kufungua Mkutano wa nane wa YouthConnekt Africa jijini Kigali, Rwanda, Novemba 25, 2026. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)
KIGALI - Mkutano wa nane wa YouthConnekt Africa umefunguliwa rasmi jana Jumatano katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, ukihimiza vijana wa bara hilo kumiliki mipango inayounda mustakabali wao wa siku za baadaye.
Vijana zaidi ya 3,000, vilevile viongozi kutoka sekta ya umma na binafsi kote barani Afrika, wamehudhuria mkutano huo unaofanyika chini ya kaulimbiu ya "Kutengeneza Jukumu la Kizazi."
Mkutano huo wa siku tatu, unaoendelea hadi Ijumaa, unatoa jukwaa kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kujenga ushirikiano.
Katika hotuba yake, Rais wa Rwanda Paul Kagame amewahimiza vijana kutumia vema fursa zilizotengenezwa kwa ajili yao.
"Mafanikio ya kweli huanza pale unapojenga maisha unayoyataka kwa ajili yako mwenyewe, bila kusubiri ruhusa ya mtu yeyote. Kila kitu ambacho Afrika imefanikiwa kujenga hadi sasa kimepatikana pale tunapomiliki mustakabali wetu wenyewe," amesema.
Kagame amesisitiza umuhimu wa ushirikiano pamoja na kunufaishana katika uhusiano kati ya viongozi na vijana wa Afrika.
Pia amesema kuwa vijana wanapaswa kubainisha jukumu lao bila kusubiri kupewa misaada katika kuunda mustakabali wao.
Matthias Naab, Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kikanda kwa Afrika cha Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), amesema vijana wa Afrika hawahitaji tu mipango mbalimbali, bali pia wanahitaji "mazingira ambayo yanaunganisha mawazo na matarajio yao na upatikanaji wa fedha, masoko, fursa za uongozi na matokeo ya kudumu."
Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2017, YouthConnekt Africa imekua na kuwa vuguvugu la kuleta mabadiliko makubwa katika bara zima, ikijiweka kama mojawapo ya majukwaa makubwa na yenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika kwa ajili ya kuwawezesha vijana, kuhimiza uvumbuzi, na kushirikisha katika masuala ya sera, kwa mujibu wa maafisa.
Mpango huo wa Afrika zima kwa sasa unatekelezwa katika nchi 39, ukiwa na lengo la kuwawezesha vijana kupitia ukuzaji wa uongozi, maendeleo ya ujuzi, ujasiriamali, na ushirikishaji wa raia.

Viongozi vijana, wavumbuzi, na waleta mabadiliko kutoka barani Afrika wakihudhuria Mkutano wa nane wa YouthConnekt Africa jijini Kigali, Rwanda, tarehe 25 Novemba 2026. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)

Rais wa Rwanda Paul Kagame akitoa hotuba yake kwenye hafla ya kufungua Mkutano wa nane wa YouthConnekt Africa jijini Kigali, Rwanda, Novemba 25, 2026. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua)

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China

Shughuli ya Siku ya Meli ya "Xuelong 2" ya China kufunguliwa kwa umma yafanyika Hainan
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma