Lugha Nyingine
Jumuiya ya Urafiki kati ya Misri na China yaadhimisha miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia

Wageni wakihudhuria hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, jijini Cairo, Misri, Novemba 24, 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)
CAIRO – Jumuiya ya Urafiki kati ya Misri na China iliandaa hafla jijini Cairo jioni ya Jumanne wiki hii kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, pamoja na miaka 77 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu wa zamani wa Misri, Essam Sharaf, alisema kuwa maadhimisho hayo hayakuwa tu njia ya kukumbuka yaliyopita, bali pia fursa ya kutafakari kuhusu urithi ambao nchi hizo mbili zinatumai kuukabidhi kwa vizazi vijavyo.
Alielezea matumaini kwa ushirikiano wa kina zaidi katika elimu, utafiti wa kisayansi na uvumbuzi, vilevile mabadilishano mapana zaidi miongoni mwa vijana, taasisi za kitamaduni, na makundi ya asasi za kiraia.
Balozi wa China nchini Misri, Liao Liqiang, alisema kuwa katika miongo saba iliyopita, uhusiano kati ya China na Misri umeweza kuhimili changamoto mbalimbali na kujenga sifa za kipekee za usawa na kuaminiana, urafiki na kufunzana, mshikamano na kuungana mkono, vilevile ushirikiano wa kunufaisha pande zote mbili.
Ali El-Hefny, Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Urafiki kati ya Misri na China, alisema kuwa nguvu ya uhusiano wa pande mbili siyo tu ipo katika upana wa ushirikiano, bali pia katika maono na kanuni ambazo nchi hizo zote zinazo.
Alisema kuwa mazungumzo kati ya Misri na China yanatoa mfano bora kwa uhusiano miongoni mwa mataifa, yakidhihirisha moyo wa kuheshimiana na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili.
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri, Mohamed al-Orabi, ameliambia shirika la habari la China, Xinhua kuwa hadhi ya nchi hizo mbili ya kuwa mataifa yenye ustaarabu wa kale na urithi mkubwa wa kihistoria imeweka msingi imara kwa uhusiano wa pande mbili.
Pia amepongeza kuongezeka kwa mazungumzo na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili juu ya masuala mbalimbali, ikiwemo suala la Palestina, rasilimali za maji, maendeleo, na ujenzi wa mambo ya kisasa.
Hafla hiyo ilijumuisha onesho la filamu ya makala kuhusu maendeleo ya uhusiano wa pande hizo mbili, pamoja na maonesho ya sanaa yaliyowasilishwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Misri.
Maonesho ya picha pia yaliandaliwa katika eneo hilo, yakionesha historia ya uhusiano kati ya China na Misri pamoja na juhudi za jumuiya hiyo katika kuhimiza mabadilishano ya kati ya serikali na yale ya kati ya watu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1958.

Balozi wa China nchini Misri, Liao Liqiang, akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, jijini Cairo, Misri, tarehe 24 Novemba 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

Balozi wa China nchini Misri, Liao Liqiang (katikati), na Waziri Mkuu wa zamani wa Misri, Essam Sharaf (wa pili kutoka kushoto), wakitembelea maonesho ya picha kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, jijini Cairo, Misri, tarehe 24 Novemba 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

Wageni wakihudhuria hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, jijini Cairo, Misri, tarehe 24 Novemba 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

Waziri Mkuu wa zamani wa Misri, Essam Sharaf, akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Misri, jijini Cairo, Misri, tarehe 24 Novemba 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

Urejeshaji ikolojia waleta uoto wa kijani kwenye kando za Mto Changjiang huko Wuhan, China

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma