Tanzania yatenga dola za kimarekani milioni 39.1 kufufua utalii ulioathiriwa na Janga la UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 18, 2021

DAR ES SALAAM - Tanzania imetenga shilingi bilioni 90.6 za kitanzania (karibu dola kimarekani milioni 39.1) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 23 inayolenga kufufua sekta ya utalii iliyoathiriwa na janga la UVIKO-19.

Damas Ndumbaro, Waziri wa Maliasili na Utalii wa nchi hiyo, amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika Mjini Dar es Salaam kwamba, fedha hizo ni sehemu ya dola za kimarekani milioni 567.25 zilizoidhinishwa mwezi Septemba mwaka huu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

IMF iliidhinisha fedha hizo kwa msaada wa dharura wa kifedha kwa Tanzania chini ya Mfumo wa Utoaji wa Mikopo na utoaji wa fedha wa Haraka unaounga mkono juhudi za nchi mbalimbali katika kukabiliana na janga hilo kwa kushughulikia athari za afya, hali ya binadamu na uchumi.

Ndumbaro amesema, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu, uanzishaji wa mifumo ya usalama, ununuzi wa vifaa vinavyotembea kwa ajili ya kuwapima watalii maambukizi ya UVIKO-19 na ununuzi wa vifaa vya usafirishaji.

"Miradi hii itarahisisha kufikika kwa vivutio tofauti vya utalii na baadaye kufufua sekta ya utalii," amesema Waziri huyo.

Ameongeza kuwa, sehemu ya fedha hizo zitatumika kukarabati barabara zinazoelekea katika mbuga za Serengeti, Mkomazi, Tarangire, Nyerere, Kilimanjaro, Saadani na Gombe. Aidha, fedha hizo pia zitatumika kuhifadhi misitu inayosimamiwa na Wakala wa Serikali wa Huduma za Misitu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha