Mwakilishi wa China atoa mwito wa kukabiliana na usafirishaji wa silaha ndogo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 23, 2021

UMOJA WA MATAIFA, New York - Mjumbe wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun, ametoa mwito wa kuchukua hatua za kina ili kukabiliana na usafirishaji wa silaha ndogo na nyepesi.

Akizungumza Jumatatu ya wiki hii kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama kuhusu silaha ndogo na nyepesi, Zhang amesema, udhibiti wa silaha ndogo na nyepesi unahusisha amani na usalama. Kupambana na usafirishaji haramu wa silaha ni muhimu sana katika kulinda maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi zote. Kwa hivyo, ni jambo la muhimu kwa kuimarisha udhibiti wa silaha ndani ya mfumo wa pande nyingi.

Amebainisha kwamba, kwa miaka mingi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya jitihada zisizo na kikomo kukabiliana na suala hilo. Baraza lilipitisha Maazimio ya Na. 2117 na Na. 2220 na limezingatia kwa ujumla athari za silaha ndogo na nyepesi wakati wa kujadili masuala nyeti ya kikanda.

Zhang amesema, biashara haramu ya silaha ndogo na nyepesi bado ni tatizo kubwa ambalo linafungamana na migogoro ya kivita, ugaidi, uhalifu wa kuvuka mipaka na matishio mengine yanayozidisha mateso ya watu katika maeneo yenye migogoro na kuleta changamoto kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.

Ameishauri Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia katika maeneo manne: kuimarisha ujenzi wa uwezo wa nchi husika na kufikia usimamizi kamili wa silaha ndogo na nyepesi, kusaidia nchi za kikanda kutimiza ufufukaji wa uchumi baada ya UVIKO-19 na kushughulikia sababu kuu za migogoro na vurugu, kutekeleza kikamilifu vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama na kukata mnyororo wa usafirishaji haramu wa silaha ndogo na nyepesi, na kuimarisha ushirikiano wa kivitendo wa pande nyingi na wa pande mbili na kuinua kikamilifu jukumu la Umoja wa Mataifa likiwa njia kuu.

Amebainisha kuwa, sababu kuu za usafirishaji haramu wa silaha ndogo na nyepesi ni umaskini na maendeleo duni. Inapaswa kuzingatia maendeleo ya kiuchumi na maisha ya watu katika maeneo yenye vita na nchi zilizo na vita, hasa kusaidia nchi zinazohusika katika kuondoa umaskini wa muda mrefu na hali ya kuwa nyuma kimaendeleo.

Amesisitiza kuwa, ni muhimu kusaidia nchi zinazoendelea kuimarisha maendeleo ya miundombinu, kuharakisha mchakato wa maendeleo ya viwanda na kisasa, kufikia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi, na kudumisha amani ya kudumu ya kikanda.

Ameongeza kwamba, maazimio husika yanapaswa kutafsiriwa kwa usahihi na kutekelezwa kwa ufasaha. Na utekelezaji wa vikwazo hivyo havipaswi kuchukuliwa kuwa kisingizio cha kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi husika au kukiuka mamlaka yao.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha