China yatuma wahudumu wa afya 40,000 huko Shanghai huku ikisisitiza sera ya “maambukizi sifuri ya UVIKO”

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 07, 2022
China yatuma wahudumu wa afya 40,000 huko Shanghai huku ikisisitiza sera ya “maambukizi sifuri ya UVIKO”
Picha iliyopigwa Aprili 3, 2022 ikionesha wahudumu wa afya wakiondoka katika Kituo cha Reli cha Magharibi cha Tianjin, Kaskazini mwa China kuelekea Shanghai ili kusaidia mji huo kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya Korona. (Xinhua/Li Ran)

SHANGHAI - Zaidi ya wahudumu wa afya 38,000 kutoka mikoa 15 ya China wameelekea Mji wa Shanghai, kituo muhimu cha biashara cha China kusaidia katika mapambano yake dhidi ya kuzuka tena kwa UVIKO-19.

Kwa mujibu wa Kamati ya Afya ya Taifa ya China (NHC), wahudumu wa afya 27,000 wanawajibika kwa kazi ya kuchukua sampuli na upimaji wa virusi vya Korona na wengine 11,000 wanafanya kazi katika hospitali za muda.

Siku ya Jumanne wiki hii Shanghai iliripoti maambukizi ya ndani ya korona yapatayo 311 na maambukizi yasiyoonesha dalili nyingi 16,766.

Takwimu kutoka Idara ya Afya ya Shanghai zinaonesha kuwa, tokea Machi Mosi, takriban watu 90,000 wameambukizwa virusi vya Korona aina ya Omicron vinavyoambukiza sana.

Kituo cha Reli cha Hongqiao cha Shanghai kilianza tena pilikapilika za shughuli nyingi katika siku chache zilizopita, huku treni nyingi zikiwa zimebeba maelfu ya wahudumu wa afya na tani za vifaa vya kukabiliana na janga hilo zikiingia. Kati ya Aprili 3 na 4, jumla ya safari 26 za ndege maalumu kutoka mikoa saba ya China zilitua katika viwanja vya ndege viwili vikubwa vya Shanghai.

Naibu Waziri Mkuu wa China Sun Chunlan Jumamosi ya wiki iliyopita alihimiza hatua madhubuti na za haraka kukomesha haraka iwezekanavyo kuenea kwa maambukizi ya virusi vya korona huko Shanghai.

"Ni kazi ngumu na changamoto kubwa kupambana na maambukizi ya virusi vya Korona aina ya Omicron huku tukidumisha utendakazi wa kawaida wa kazi muhimu katika mji mkubwa wenye wakazi milioni 25," Sun alisema.

Shanghai, moja ya miji mikubwa nchini China iko chini ya usimamizi wa muda wa kufungwa. Baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji wa antijeni siku ya Jumapili ya wiki iliyopita na kupima virusi vya Korona katika mji mzima siku ya Jumatatu wiki hii, Jana Jumatano Shanghai imeanzisha duru mpya ya upimaji wa virusi vya korona kwa wakaazi wote ikiwa ni sehemu ya juhudi mpya za kukomesha maambukizi katika jamii na kudhibiti maambukizi ya korona.

Zaidi ya maeneo 60, likiwemo eneo la Maonyesho ya Kimataifa ya Shanghai na Kituo cha Mikutano lenye zaidi ya mita za mraba 150,000, yamebadilishwa kuwa maeneo yenye hospitali za muda.

Mapema jana Jumatano Msemaji wa Kamati ya Taifa ya Afya ya China (NHC) alisema kuwa, pamoja na maambukizi ya korona kuendelea kuongezeka, China itaendelea kufuata sera yake ya “maambukizi sifuri ya UVIKO”.

China Bara Jumanne wiki hii lilirekodi maambukizi ya ndani ya korona yapatayo 1,383 na waathirika wa virusi vya Korona wasioonesha dalili nyingi 19,089. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha