China imetoa zaidi ya dozi bilioni 2.2 za chanjo dhidi ya UVIKO kwa Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2022

Picha iliyopigwa Machi 29, 2022 ikionyesha vifurushi vya chanjo dhidi ya UVIKO-19 aina ya Sinovac kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Phnom Penh huko Phnom Penh, Cambodia. (Picha na Ly Lay/Xinhua)

BEIJING – Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, China imetoa zaidi ya dozi bilioni 2.2 za chanjo dhidi ya Virusi vya Korona (UVIKO-19) kwa zaidi ya nchi na mashirika ya kimataifa 120 hadi kufikia jana Jumatano, nchi nyingi zilizopokea msaada huo zikiwa ni zile zinazoendelea.

China ilikuwa ya kwanza kuunga mkono kuacha hakimiliki ya ubunifu kwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kufanya ushirikiano wa uzalishaji wa chanjo na nchi zingine zinazoendelea. Hadi sasa, China imefanya ushirikiano wa uzalishaji wa chanjo na nchi 13 na kusaini makubaliano ya ushirikiano na nchi nane.

Tangu kuzuka kwa janga la UVIKO-19, China imetekeleza hatua za dharura za kibinadamu duniani kwa kutoa kiasi kikubwa zaidi cha chanjo dhidi ya janga hilo, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Jamhuri ya Watu wa China.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kwa Shirika la Habari la China, Xinhua, hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, China kwa ujumla imetoa vifaa tiba vya kupambana na UVIKO kwa nchi 153 na mashirika 15 ya kimataifa, yakiwemo mavazi maalumu ya kujikinga na virusi yapatayo bilioni 4.6 na barakoa zaidi ya bilioni 430.

China pia imetuma timu 37 za wahudumu wa afya katika nchi 34 na kutoa uzoefu wa kuzuia na kudhibiti janga hilo kwa zaidi ya nchi na mashirika ya kimataifa 180.

Kwa kuwa China imeshiriki kikamilifu katika mipango ya COVAX na ACT-A chini ya mfumo wa Shirika la Afya Duniani, China hadi sasa imetoa dola za kimarekani milioni 100 kwa COVAX kwa ajili ya usambazaji wa chanjo kwa nchi zinazoendelea.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha