Ubalozi wa China waanzisha mpango wa vyombo vya habari kuhimiza amani ya Sudan Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 13, 2022

JUBA –Shirikisho la Waandishi wa Habari la Sudan Kusini na Ubalozi wa China nchini humo Alhamisi wiki hii vilianzisha mradi wa ripoti wenye kaulimbiu ya "Amani Yangu" ukiwa na lengo la kusambaza ujumbe wa amani na kuhimiza ushiriki wa watu wengi, kwa msaada wa Wizara ya Ujenzi wa Amani ya Sudan Kusini.

Stephen Par Kuol, Waziri wa Ujenzi wa Amani wa Sudani Kusini, amesema kuna haja ya kufanya juhudi za kuionyesha dunia hali ilivyo ya nchi hiyo baada ya mgogoro wa miaka mingi kumalizika na kusaini makubaliano ya kujenga upya hali ya amani ya nchi hiyo Mwaka 2018.

"Sudan Kusini inatoka katika vita na vita vilikuwa nasi kwa muda mrefu sana, tulimaliza tu vita vya kujipatia uhuru wa nchi hii kisha tukaingia kwenye vita vingine," Par alisema wakati wa kuanzishwa kwa mradi wa "Amani Yangu" huko Juba, Mji Mkuu wa Sudan Kusini.

Par alisema kukumbatia makubaliano ya amani ni muhimu katika kubadilisha fikra za wakazi wa Sudan Kusini ambao wameumizwa na vita vya miongo kadhaa.

"Nadhani ni hatua ya kimaendeleo katika mwelekeo sahihi kwamba vyombo vya habari siyo tu vinaripoti mgogoro wa Sudan Kusini, vita na migogoro lakini pia maendeleo ya hali ya mambo ," amesema waziri huyo. Akibainisha kuwa baraza la mawaziri la nchi hiyo hivi karibuni lilipitisha azimio la kuendeleza amani nchini Sudan Kusini, na kuongeza kuwa vyombo vya habari vitakuwa mhimili muhimu katika kusambaza ujumbe wa amani.

Oyet Patrick Charles, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanahabari wa Sudan Kusini (UJOSS), amehimiza mashirika ya vyombo vya habari kuipa kipaumbele ajenda ya kukuza amani ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Balozi wa China nchini Sudan Kusini Hua Ning amesema nchi hiyo changa zaidi duniani imeshuhudia maendeleo katika mchakato wa amani ambayo yamepelekea kuimarika kwa uchumi.

Alisisitiza kuwa licha ya changamoto zinazoendelea katika mchakato wa amani, mabadiliko yenye matumaini ni dhahiri kwa wote.

"Kama mfuasi, mshiriki na mchangiaji wa mchakato wa amani ya Sudan Kusini, ubalozi wa China unatumai kuwa mradi wa 'Amani Yangu' utahimiza amani na imani ya watu wa Sudan Kusini katika amani, kuwahimiza kushiriki vyema katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo. Kufikia hatua ya utulivu wa muda mrefu wa nchi huku wakiboresha maisha yao kwa kufanya kazi kwa bidii," Balozi wa China amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha