Misri yazindua ugunduzi wa majeneza ya kale 250 na sanamu za kale 150 huko Saqqara

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 31, 2022
Misri yazindua ugunduzi wa majeneza ya kale 250 na sanamu za kale 150 huko Saqqara
Picha iliyopigwa Mei 30, 2022 ikionyesha majeneza yenye rangi mbalimbali yakiwa na maiti za kale zilizotiwa mumiani ndani yake wakati wa maonyesho ya mafanikio ya kiakiolojia huko Saqqara necropolis, Kusini mwa Cairo, Misri. Misri siku ya Jumatatu wiki hii ilizindua ugunduzi mkubwa mpya wa kiakiolojia wa majeneza 250 yaliyofungwa yakiwa na zake zilizotiwa mumiani, sanamu 150 za shaba za miungu ya kale ya kiume na ya kike, na vitu vingine vya kale huko Saqqara necropolis, Kusini mwa Cairo. (Xinhua/Sui Xiankai)

CAIRO - Misri Jumatatu wiki hii imezindua ugunduzi mkubwa mpya wa kiakiolojia wa majeneza ya kale 250 yaliyofungwa yakiwa na maiti za kale zilizotiwa mumiani ndani yake, sanamu 150 za shaba za miungu ya kale ya kiume na ya kike, na vitu vingine vya kale katika eneo la Saqqara, Kusini mwa Mji Mkuu Cairo.

Mostafa Waziri, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Mambo ya Kale la Misri, ameviambia vyombo vya habari kwamba, ujumbe wa wanaakiolojia wa Misri unaofanya kazi katika eneo la Makaburi ya Bubastian uligundua hifadhi ya sanamu za shaba kwenye eneo ambalo lilianzishwa wakati wa Enzi ya Misri ya kale.

"Hifadhi hiyo ilijumuisha sanamu 150 zenye saizi tofauti za shaba za miungu ya kale ya kiume na ya kike ikiwemo Anubis, Amunmeen, Osiris, Isis, Nefertum, Bastet, Hathor, na vyungu kadhaa vya shaba," Waziri amesema.

Ameongeza kuwa, ujumbe huo pia umegundua majeneza 250 yaliyotengenezwa kwa mbao na yenye rangi mbalimbali ambayo ni ya kipindi cha miaka 500 K.K. ndani ya visima kadhaa vya kuzikia yakiwa na maiti za kale zilizotiwa mumiani na kuhifadhiwa vizuri pamoja na kundi la sanamu zilizochongwa kwa mbao zenye uso wa dhahabu, masanduku ya mbao yaliyopakwa rangi, na hirizi.

Waziri amesema, wakati wa kazi ya uchimbaji ndani ya kisima kimoja, ujumbe huo ulipata mafunjo ambayo yana maandishi ya aya za Kitabu cha Wafu.

Mkusanyiko wa vipodozi pia ulipatikana, ikiwa ni pamoja na masega, kope, kontena, bangili, pete, na shanga za mbegu.

“Ugunduzi huo ulifanywa wakati wa uchimbaji wa awamu ya nne wa eneo hilo ulioanza Aprili 2018. Ujumbe wa Misri utaanza kazi ya awamu ya tano ya uchimbaji Mwezi Septemba mwaka huu”, Waziri ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha