

Lugha Nyingine
Zambia yazindua kituo cha kisasa cha mikutano kilichofadhiliwa na China
LUSAKA - Zambia Jumanne wiki hii imezindua kituo cha kisasa cha mikutano cha kimataifa kilichofadhiliwa na China.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenneth Kaunda, chenye ukumbi wake mkuu wenye uwezo wa kuchukua watu 2,500, kimejengwa kwa ajili ya kutumika kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) wa katikati ya mwaka huu.
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameishukuru China kwa zawadi hiyo nzuri, na kusema kuwa Serikali ya Zambia inashukuru kwa msaada uliotolewa katika maendeleo ya miundombinu ya nchi hiyo toka miaka ya 1970 kupitia ujenzi wa Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA).
"Hili lilikuwa jambo muhimu katika historia yetu, wakati Zambia haikuwa na njia ya kuifikia bahari, kwa hiyo haikuweza kuagiza au kuuza nje bidhaa kutokana na vizuizi vya Rhodesia Kusini (Zimbabwe ya leo)," amesema.
Amesema, kituo hicho cha mikutano kitachangia katika kuifanya Zambia kuwa kitovu cha kuandaa vikao na mikutano ya kimataifa. Pia amempongeza mkandarasi wa China kwa kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa.
Rais wa Zambia amewaalika Wachina kwa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa miradi ya miundombinu inajengwa kwa bei sahihi na kuwasilishwa kwa ubora na wakati uliopangwa.
“Zambia ilikuwa inatazamia ukurasa mpya wa kuimarishwa kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili ili kuboresha maisha ya watu wa nchi hizo mbili”, amesema Hichilema.
Kwa upande wake Du Xiaohui, Balozi wa China nchini Zambia, amesema ujenzi wa mradi huo unaonyesha kuongezeka kwa uhusiano wa kindugu uliokuwepo kati ya nchi hizo mbili.
Ameipongeza Zambia kwa kukamilisha kwa mafanikio mradi huo unaodhihirisha moyo wa uhusiano kati ya China na Zambia ulioanzishwa na viongozi waasisi wa nchi hizo mbili.
Du amesema mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuisaidia Zambia kuinua hadhi yake ya kimataifa na pia kuwezesha taifa hilo la Kusini mwa Afrika kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Jiangsu ya China, Tawi la Zambia, Wang Shulin, amesema ni heshima kwa kampuni hiyo kupewa fursa ya kujenga na kukamilisha mradi huo.
Amesema kampuni hiyo imeweza kujenga mradi huo kwa kuzingatia viwango vya usalama na mazingira licha ya changamoto zilizoletwa na janga la UVIKO-19.
Ujenzi wa kituo hicho cha mikutano ulianza Mwaka 2020.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma