Idadi ya vifo vya wahamiaji waliopatikana ndani ya tela la lori huko Texas Marekani yafikia 50

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 29, 2022
Idadi ya vifo vya wahamiaji waliopatikana ndani ya tela la lori huko Texas Marekani yafikia 50
Picha iliyopigwa Juni 27, 2022 ikionyesha eneo ambalo inadhaniwa ni la tukio la kusafirisha watu wengi kimagendo ambao walikutwa wamefariki huko San Antonio, Texas, Marekani. Mamlaka zilisema Jumanne kwamba, idadi ya vifo vya wahamiaji waliopatikana ndani ya lori lenye tela la magurudumu 18 na kutelekezwa huko San Antonio, Marekani Jumatatu wiki hii imeongezeka na kufikia watu 50. (Picha na Nick Wagner/Xinhua)

HOUSTON - Idadi ya vifo vya wahamiaji waliopatikana ndani ya tela la lori "la kutengenezwa" lenye magurudumu 18 huko San Antonio, mji mkubwa katika Jimbo la Texas Kusini-Kati mwa Marekani imeongezeka hadi kufikia 50.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, mkasa huo unaonekana kuwa moja ya matukio mabaya zaidi ya magendo ya wahamiaji katika historia ya hivi karibuni ya Marekani.

Redio ya Umma ya Texas iliripoti, ikimnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico Marcelo Ebrard akisema kuwa, watu 46 walikutwa wamefariki katika eneo la tukio na wengine wanne walitangazwa kufariki katika hospitali za eneo hilo.

Ebrard amesema watu 22 kati ya hao waliofariki ni raia wa Mexico, saba kutoka Guatemala, wawili kutoka Honduras, na wengine 19 bado hawajatambuliwa.

Takriban watu wengine wasiopungua 16 waliokutwa katika tela hilo, wakiwemo watoto wanne, walipelekwa katika hospitali za eneo hilo kutokana na kuzidiwa na joto na upungufu wa maji mwilini, maafisa wa eneo hilo walisema katika mkutano na wanahabari. Takriban watu 100 waliripotiwa kupakiwa ndani ya tela hilo lenye magurudumu 18.

Gazeti la San Antonio Express-News liliripoti kwamba mtu fulani "alitengeneza" tela hilo lililokuwa limewabeba wahamiaji hao na kulipaka rangi na kuweka nambari zinazofanana na za Idara ya Usafiri ya Marekani na ile ya Jimbo la Texas ili lionekane kama lori linalomilikiwa na kampuni ya malori ya Kusini mwa Texas katika jitihada za kukwepa kukamatwa na mamlaka.

Mkuu wa Polisi wa San Antonio William McManus aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa Jumatatu usiku kuwa, watu watatu wako chini ya ulinzi wa polisi, lakini haijulikani kama walihusika katika mkasa huo.

McManus alisema Polisi walipokea simu Jumatatu jioni kutoka kwa mtu anayefanya kazi karibu, ambaye alisikia vilio vya kuomba msaada kutoka kwenye tela hilo Kusini Magharibi mwa mji huo, walikaribia na kuona miili ndani ya tela na milango yake ikiwa wazi.

Gavana wa Texas kupitia chama cha Republican Greg Abbott, ambaye anawania muhula wa pili, Jumatatu usiku alimlaumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa mkasa huo, akiandika kupitia Twitter: "Vifo hivi vinamkabili Biden. Ni matokeo ya sera zake mbaya za kuacha mpaka wazi."

Julai 2017, wahamiaji 10 walikufa kwenye lori lililokuwa limebeba watu 39 huko San Antonio. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha