China yaitaka Marekani kuacha kupora rasilimali za taifa nchini Syria

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 21, 2022

(Picha inatoka Xinhua.)

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin Jumatano wiki hii amesema kuwa Marekani inapaswa kuacha mara moja kupora rasilimali za taifa nchini Syria.

Wang aliyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ripoti kwamba hivi karibuni majeshi ya Marekani yanayokalia kwa mabavu maeneo ya Syria yalihamisha mafuta yaliyokuwa yameibwa kutoka Syria kwenda Kaskazini mwa Iraq, huku maafisa wa Syria wakiilaani Marekani na washirika wake kwa kufanya kama maharamia.

Wang amesema kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Syria kwa sasa wanaishi chini ya mstari wa umaskini, theluthi mbili ya watu wa nchi hiyo wanategemea msaada wa kibinadamu, na zaidi ya nusu ya watu wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

“Jeshi la Marekani bado linashikilia maeneo muhimu ya uzalishaji wa nafaka na mafuta nchini Syria, kupora na kuiba rasilimali za taifa nchini Syria, na kuzidisha misukosuko ya kibinadamu katika eneo hilo,” Wang amesema, huku akiongeza kuwa baadhi ya watu wa Syria wameelezea uwepo wa Marekani nchini Syria kama aina ya ugaidi.

Wang amesema Marekani daima imekuwa ikijivunia juu ya kile kinachoitwa viwango vya juu zaidi vya haki za binadamu na utawala kwa mujibu wa sheria, lakini hatua za Marekani nchini Syria zinathibitisha kwamba kweli inashindwa katika mambo haya.

“Marekani inapaswa kuheshimu mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya Syria, kuitikia wito wa watu wa Syria, kuondoa mara moja vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Syria, kuacha mara moja kupora rasilimali za taifa nchini Syria, na kufidia kwa vitendo madhubuti madhara yaliyowapata watu wa Syria” amesema Wang.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha