Reli ya Ethiopia-Djibouti yaanza usafirishaji wa magari

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 26, 2022
Reli ya Ethiopia-Djibouti yaanza usafirishaji wa magari
Kichwa cha Treni kikionekana kwenye viunga vya Addis Ababa, Ethiopia, Agosti 25, 2022. Reli ya Ethiopia-Djibouti iliyojengwa na China Alhamisi wiki hii imeanza usafirishaji wa magari kutoka bandarini nchini Djibouti hadi Addis Ababa, Mji Mkuu wa Ethiopia. Shehena ya kwanza ya magari iliwasili katika Kituo cha Mizigo cha Indode nje kidogo ya Addis Ababa. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA - Reli ya Ethiopia-Djibouti iliyojengwa na China Alhamisi wiki hii imeanza usafirishaji wa magari kutoka bandarini nchini Djibouti hadi Addis Ababa, Mji Mkuu wa Ethiopia.

Shehena ya kwanza ya magari iliwasili katika Kituo cha Mizigo cha Indode nje kidogo ya Addis Ababa.

Hafla maalum imefanyika kituoni hapo kuashiria kuwasili kwa shehena ya kwanza.

Abdi Zenebe, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ubia la Reli ya Ethiopia-Djibouti (EDR), amepongeza hatua hiyo, akisisitiza kwamba itasaidia kutimiza matarajio makubwa ya reli hiyo katika suala la kuwezesha mfumo wa usafirishaji wa Ethiopia.

Akibainisha usafirishaji mkubwa wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya Ethiopia kutoka bandari za Djibouti hadi katikati mwa Ethiopia na bidhaa zinazosafirishwa kutoka Ethiopia hadi kwingineko duniani kupitia bandari za Djibouti, Zenebe amesema shehena hiyo ya kwanza kabisa ya magari kutoka Djibouti hadi Ethiopia inaashiria dhamira ya EDR ya kubadilisha huduma zake za usafiri.

"Hii inaonyesha kwamba tunabadilisha biashara zetu. Tuna aina nyingi za mabehewa, ambayo ni pamoja na hoppers, tuna mabehewa yenye friji, tuna idadi kubwa ya mabehewa ambayo bado hatujajayatumia," Zenebe amesema.

"Hii ni njia mojawapo ya kuonyesha na kuiambia Dunia na wateja wetu kwamba tumeanza kutumia mabehewa haya (ya reli), na mseto na upanuzi huu wa biashara utahakikisha maendeleo ya EDR katika siku zijazo na utapanua huduma ya EDR kwa nchi hizo mbili na wateja wanaohusika."

Reli hiyo ya Ethiopia-Djibouti yenye urefu wa kilomita 752.7, inayojulikana pia kwa jina la reli ya Addis Ababa-Djibouti, iliyojengwa kwa kandarasi ya Kampuni za China Rail Engineering Corporation (CREC) na China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), ni reli ya kwanza ya kisasa ya kuvuka mipaka katika Bara la Afrika.

Wakati reli ya hiyo ya kutumia umeme ya Ethiopia-Djibouti inaboresha kwa kiasi kikubwa soko la mizigo, EDR imesema reli hiyo inaboresha huduma zake, kuelekea kutimiza azma ya nchi hizo mbili ya kujenga ukanda wa viwanda na uchumi unaochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hizo mbili.

Abdurahman Ibrahim, Meneja Mkuu wa Nana Solutions, kampuni ambayo imeshirikiana na EDR kuagiza shehena hiyo ya kwanza ya magari 24 kupitia reli ya Ethiopia-Djibouti, amesema reli hiyo inatoa faida mbalimbali kwa makampuni yanayojihusisha na sekta ya uingizaji nchini na uuzaji nje wa bidhaa.

"Tuna bahati sana kuwa watangulizi katika mpango huu mzuri sana. Unatoa fursa mbalimbali kwetu, ikiwa ni pamoja na usalama kwani kutumia mabehewa ya reli kuna ulinzi na usalama wa hali ya juu hadi mwisho wake," Ibrahim ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua huku akiongeza kuwa usafiri huo unapunguza gharama kwa karibu nusu ikilinganishwa na malori ya kubeba magari. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha