Upigaji kura wamalizika katika uchaguzi wa rais nchini Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 13, 2023
Upigaji kura wamalizika katika uchaguzi wa rais nchini Misri
Wafanyakazi wakihesabu kura baada ya kukamilika kwa upigaji kura katika uchaguzi wa rais nchini Misri kwenye kituo cha kupigia kura huko Cairo, Misri, Desemba 12, 2023. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO – Mamlaka ya Uchaguzi ya kitaifa ya Misri (NEA) imesema, Misri imehitimisha mchakato wa upigaji kura wa siku tatu Jumanne katika uchaguzi wa rais huku mchakato wa kuhesabu kura ukiwa umeanza mara moja, ambapo ratiba iliyotolewa hapo awali na NEA inaonyesha kuwa mchakato wa kuhesabu kura, ambao ulianza baada ya 3:00 usiku kwa saa za Misri (1900 GMT) siku ya Jumanne, utakamilika leo Jumatano.

"Idadi ya wapiga kura katika siku ya tatu ni kubwa bila kutarajiwa, ikionyesha kujitokeza kwa wapiga kura wengi katika historia na ambako hakujawahi kutokea," Mkurugenzi Mtendaji wa NEA Ahmed Bendari amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari, akisema idadi hiyo kubwa ya wapiga kura inatokana na kuongezeka kwa uelewa wa uraia.

Mamlaka hiyo imesema, idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura siku ya Jumatatu ilifikia asilimia takriban 45 ya jumla ya wapiga kura wote halali milioni 67.

Upigaji kura kwenye uchaguzi huo wa urais ulianza Jumapili nchini Misri huku wagombea wanne wakichuana, akiwemo Rais aliye madarakani Abdel-Fattah al-Sisi, ambaye anawania muhula wa tatu kama inavyoruhusiwa kipekee na marekebisho ya katiba ya Mwaka 2019, ambayo pia yameongeza muda wa urais kutoka miaka minne hadi sita. Alishinda chaguzi zote mbili za Mwaka 2014 na 2018 kwa kura nyingi.

Wagombea wengine watatu ni Farid Zahran wa Chama cha Social Democratic, Abdel-Sanad Yamama wa Chama cha Al-Wafd na Hazem Omar wa Chama cha People's Republican.

Uchaguzi wa rais wa Misri unategemea mfumo wa “kura nyingi-duru mbili za uchaguzi”, ambapo mmoja wa wagombea lazima ashinde kura nyingi zenye kumpa ushindi wa moja kwa moja ili kuepuka uchaguzi kwenda duru ya pili.

Matokeo ya mwisho yamepangwa kutangazwa rasmi Desemba 18, na iwapo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi, itatangazwa Januari 16, 2024, kwa mujibu wa NEA.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha