

Lugha Nyingine
Vijana wengi zaidi wa Tanzania wachagua masomo ya usiku ya lugha ya Kichina kama daraja la fursa za siku za baadaye (4)
DAR ES SALAAM - Jua linazama jijini Dar es Salaam, Tanzania likitoa mwanga wa rangi ya chungwa katika jiji hilo lenye pilika nyingi, mwanga wa aina tofauti huanza kumulika darasani katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo chini ya sauti ya kimnong’ono ya feni za darini, kundi la vijana Watanzania hukusanyika, wakiwemo vijana wataalamu, wajasiriamali wenye shauku, wahitimu wapya na vijana wenye shauku ya kujifunza, huku macho yao yakimwelekea mwalimu Mchina, ambaye sauti yake ni ya upole lakini yenye kujiamini.
Miongoni mwa wanafunzi hao ni mjasiriamali Rajabu Seleman Malugu, mwenye umri wa miaka 29, aliyekaa mstari wa mbele. Akiwa amevalia shati safi, huinama mbele na kalamu iliyotulia na daftari lililofunguliwa kurasa. Kwa Rajabu, kujifunza lugha ya Kichina ni zaidi ya shauku ya kitamaduni -- ni mkakati wa biashara.
“Natambua kwamba ili kupanua biashara yangu, nahitaji kuelewa lugha na utamaduni wa soko langu kubwa ambalo ni China,” amesema.
"Wachina ni wataalam wa kunadi bidhaa. Hata matangazo yao yananihamasisha. Nataka kujifunza kutoka kwao, kuzungumza lugha yao, na labda siku moja kufanya biashara nao moja kwa moja." ameongeza.
Viti vichache kutoka kwa Rajab anakaa Bhoke Juma Chacha, mhitimu wa sayansi ya viumbe vya majini mwenye umri wa miaka 25. Kwake, lugha ya Kichina inatoa lango kwa upeo mpya.
"Kujifunza Kichina si tu kuhusu lugha," amesema. "Inahusu ufikiaji -- ufikiaji wa ajira, ufikiaji safari, ufikiaji wa dunia inayothamini lugha hii." amesema.
Bhoke ana malengo yake juu ya biashara ya kimataifa au diplomasia. Lakini pia anavutiwa na uzuri wa lugha yenyewe. "Kuandika herufi za Kichina ni kama kuchora picha. Ni sanaa. Lakini pia ni changamoto. Kistari kimoja kinaweza kubadilisha maana nzima," amesema, akionyesha daftari lake lililojaa herufi zilizochorwa kwa umakini.
Mbele ya darasa, mwalimu Gao Yan husogea kati ya safu za viti. Katika darasa lake, kujifunza si mzigo bali ni safari, iliyojaa simulizi, michezo, hadithi za kitamaduni na furaha.
"Kwangu mimi, kufundisha lugha ya Kichina ni kuhusu muunganisho," amesema. "Ni kuhusu kusaidia wanafunzi wangu kuona dunia kwa njia tofauti, kuchunguza utamaduni mpya, kujenga madaraja." ameeleza.
Daraja hilo tayari linaanza kuonekana. Emmanuel Richard Legonga, mwalimu Mtanzania ambaye amekuwa akifanya kazi katika Taasisi ya hiyo ya Confucius kwa miaka minane, ameshuhudia namna wanafunzi wanavyokua kupitia programu hiyo. Wengine wamepata ajira kwenye kampuni za China nchini Tanzania; wengine wamekwenda kufundisha lugha ya Kichina wenyewe.
"Kila mwaka, idadi ya wanafunzi huongezeka. Na kila mwanafunzi ana simulizi," amesema. "Kichina si tu lugha hapa. Ni mlango wa ajira, elimu, na dunia pana." amesema.
Zhang Xiaozhen, mkurugenzi wa China wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema masomo ya hayo ya jioni yalianza mwaka 2013 na kwa sasa yapo wanafunzi 150. Amesema, kuna madarasa matano kwa ngazi ya kwanza hadi ya nne, na mihula mitano kila mwaka.
Kwa Rajabu na Bhoke na wengine wengi, Taasisi ya Confucius ni zaidi ya shule ya lugha. Ni daraja kati ya ndoto na fursa, kati ya tamaduni, na labda, siku moja, kati ya mabara.
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
Maonyesho ya Kimataifa ya Baiskeli ya China 2025 yaanza Shanghai
Shaolin Kungfu, chombo muhimu cha mawasiliano ya Utamaduni wa China na ulimwengu wa nje
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma