Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 14, 2025
Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva
Rais Xi Jinping wa China akifanya mazungumzo na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, ambaye yuko ziarani nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 13, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)

BEIJING - Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, mjini Beijing jana Jumanne, akisema kuwa kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Brazil mwaka jana, pande hizo mbili kwa pamoja zilitangaza kuinua uhusiano kati ya pande mbili kuwa jumuiya ya China na Brazil yenye mustakabali wa pamoja kwa ajili ya dunia yenye haki zaidi na sayari yenye uendelevu zaidi.

Ametoa wito kwa pande hizo mbili kusukuma mbele kwa nguvu kubwa ujenzi wa jumuiya ya China na Brazil yenye mustakabali wa pamoja, kuzidisha muunganisho wa mikakati ya maendeleo, na kwa pamoja kuhimiza mshikamano na ushirikiano kati ya Nchi za Kusini.

Rais Xi amesisitiza kuwa, China na Brazil zinapaswa kudumisha hali ya kuaminiana kimkakati, kuungana mkono juu ya masuala yanayohusu maslahi ya msingi na mambo makubwa yanayofuatiliwa na kila mmoja, na kuimarisha mawasiliano katika ngazi zote na katika mambo yote.

Ametoa wito kwa nchi hizo mbili kupanua ushirikiano, kuimarisha kuendana ipasavyo kwa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na mkakati wa maendeleo wa Brazili, kufanya kazi kikamilifu kwa jukumu la mifumo mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano katika sekta za jadi kama vile miundombinu, kilimo na nishati, na kupanua maeneo mapya ya ushirikiano katika kubadilisha muundo wa nishati, anga ya juu, uchumi wa kidigital na akili bandia.

Amesema kwamba China na Brazil zinapaswa kuongeza mawasiliano ya kitamaduni, kutoa urahisi zaidi kwa mawasiliano ya watu kati ya pande hizo mbili, na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya utamaduni, elimu, utalii na vyombo vya habari na katika ngazi za chini ya serikali kuu.

Amesisitiza kuwa, pande hizo mbili zinapaswa kutilia maanani ushirikiano wa pande nyingi, akiongeza kuwa zikiwa nchi kubwa zaidi zinazoendelea katika peo za Mashariki na Magharibi mtawalia, zinapaswa kuongeza uratibu na ushirikiano ndani ya mifumo ya pande nyingi, kushikilia ushirikiano wa pande nyingi, kuboresha usimamizi wa kimataifa, kudumisha utaratibu wa kimataifa wa kiuchumi na kibiashara, na kupinga kithabiti uamuzi wa upande mmoja, kujihami kibiashara na umwamba.

Kwa upande wa Rais Lula amesema Brazil inapenda kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na China na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya Brazil na China yenye mustakabali wa pamoja, akiongeza kuwa Brazil inapenda kuunganisha mkakati wake wa maendeleo na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja ili kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta kama vile biashara, miundombinu, anga na mambo ya fedha.

Pia ametoa wito kwa nchi hizo mbili kupanua mawasiliano katika maeneo ya vijana na utamaduni, na kuongeza mawasiliano na urafiki kati ya watu wa nchi hizo mbili.

"Kujihami kibiashara na matumizi mabaya ya ushuru haviwezi kukuza maendeleo na ustawi, badala yake, vitasababisha machafuko. Msimamo thabiti wa China katika kushughulikia changamoto duniani unazipa nguvu na hali ya kujiamini yanchi zote," Rais Lula amesema, akiongeza kuwa Brazil inapenda kuimarisha uratibu wa kimkakati na China katika masuala ya kimataifa, kushirikiana na China kulinda maslahi ya pamoja ya Nchi za Kusini na kulinda haki na usawa wa Kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha