Trump asaini mkataba mkubwa wa ulinzi na Saudi Arabia, atangaza mpango wa kuondoa vikwazo dhidi ya Syria

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 14, 2025
Trump asaini mkataba mkubwa wa ulinzi na Saudi Arabia, atangaza mpango wa kuondoa vikwazo dhidi ya Syria
Mwanamfalme wa Saudi Arabia ambaye pia ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mohammed bin Salman Al Saud (kulia) akimkaribisha Rais wa Marekani Donald Trump ambaye yuko ziarani mjini Riyadh, Saudi Arabia, Mei 13, 2025. (Shirika la Habari la Saudia/kupitia Xinhua)

RIYADH - Rais Donald Trump wa Marekani amepata ahadi ya uwekezaji wenye thamani ya dola za Kimarekani Bilioni 600 jana Jumanne kutoka Saudi Arabia mjini Riyadh na kuapa kuondoa vikwazo dhidi ya Syria ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya White House, ahadi hiyo ya uwekezaji inahusisha sekta mbalimbali, zikiwemo za "usalama wa nishati, viwanda vya ulinzi, hadhi ongozi ya kiteknolojia, na ufikiaji wa miundombinu na madini muhimu duniani.

"Miongoni mwa mikataba hiyo ni "makubaliano makubwa zaidi ya mauzo ya ulinzi katika historia -- dola za Kimarekani karibu bilioni 142," imesema taarifa hiyo.

Kama sehemu ya makubaliano ya ulinzi, Marekani itaipatia Saudi Arabia "vifaa na huduma za hali ya juu ya kupigana vita kutoka kwa kampuni zaidi ya dazeni za ulinzi za Marekani."

"Mkataba huu unawakilisha uwekezaji mkubwa katika ulinzi wa Saudi Arabia na usalama wa kikanda, uliojengwa juu ya mifumo na mafunzo ya Marekani," taarifa hiyo imeongeza.

Akizungumza baadaye kwenye baraza la uwekezaji, rais huyo wa Marekani ametangaza kwamba ataiondolea Syria vikwazo.

"Nitaamuru kusitishwa kwa vikwazo dhidi ya Syria ili kuwapa nafasi," Trump amesema, akiongeza kuwa Marekani imechukua hatua za awali kuelekea kurejesha kawaida uhusiano na Damascus.

Huku akisifu uhusiano kati yake na Saudi Arabia, Trump ameelezea matumaini kuwa nchi hiyo itajiunga na makubaliano ya Abraham. Makubaliano ya Abraham, yaliyosimamiwa na Marekani wakati wa muhula wa kwanza wa Trump madarakani, yalilenga kurejesha kawaida uhusiano kati ya Israel na nchi za Kiarabu.

Juhudi hizo za Marekani za kuhimiza urejeshaji hali ya kawaida kati ya Israel na nchi za Kiarabu zilikwama kutokana na uungaji mkono wa Marekani kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel mjini Gaza, ambayo yamesababisha Wapalestina zaidi ya 52,900 kuuawa tangu Oktoba 2023 na kupata ukosoaji mkubwa wa kikanda.

Kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine, Trump amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio atasafiri hadi Uturuki baadaye wiki hii kujiunga na mazungumzo hayo.

Trump yuko katika ziara ya siku nne Mashariki ya Kati kuanzia Jumanne hadi Ijumaa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza kubwa nje ya nchi tangu aingie madarakani Januari. Saudi Arabia ni kituo cha kwanza cha ziara yake hiyo, ambayo itajumuisha pia Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha