Kampuni ya China yasaidia kupunguza msongamano wa magari katika mji mkuu wa Guinea kwa barabara ya makutano ya ngazi tatu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2025
Kampuni ya China yasaidia kupunguza msongamano wa magari katika mji mkuu wa Guinea kwa barabara ya makutano ya ngazi tatu
Mfanyakazi akifanya kazi katika eneo la ujenzi wa Mradi wa Barabara ya Makutano ya mzunguko ya Bambeto mjini Conakry, mji mkuu wa Guinea, tarehe 29 Aprili 2025. (Xinhua/Han Xu)

CONAKRY - Huku kukiwa na msongamano mkubwa wa magari katikati ya mji wa Conakry, mji mkuu wa Guinea, muundo wa makutano ya barabara wa rangi ya manjano na nyeupe unaonekana ambapo makutano hayo ya barabara ya juu ya ngazi tatu, yanayojengwa na Shirika la Ujenzi wa Nishati la China (POWERCHINA), yamepangwa kuanza kutumika kikamilifu ifikapo mwishoni mwa Mei, ikionyesha kuwa historia ya kutokuwa na barabara za kisasa za juu katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi imeisha.

Mradi huo wa Barabara ya Makutano ya mzunguko ya Bambeto uko kwenye makutano ya Barabara ya Prince na Barabara ya T2. Eneo hili hapo awali lilikuwa likichukuliwa kuwa kizuizi kikuu cha safari za magari mjini Conakry, hasa wakati wa watu wengi wanapotumia barabara, msongamano ulikuwa mkali sana, ukifanya usafiri wa kila siku kuwa shida kubwa kwa wakazi.

Mara tu barabara hiyo ya makutano mzunguko ya Bambeto itakapofunguliwa kwa matumizi, itaondoa kizuizi hicho kikamilifu.

Gong Qiaoqi, meneja wa mradi huo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba makutano hayo yana njia ya kuvuka kwa juu, barabara ya mzunguko wa chini, na njia ya chini ya ardhi. Muundo huu unalenga kuhudumia kwa wakati mmoja magari yanayoingia na kutoka nje ya mji, usafiri kati ya maeneo, na ufikiaji haraka wa uwanja wa ndege, ukipunguza sana msongamano wa magari katika eneo hilo na maeneo yanayozunguka.

Christophe Sandouno, daktari mwenyeji, anachukulia makutano hayo ya barabara kama ni zaidi ya mradi wa barabara tu, akisema ni "kichocheo" cha maendeleo ya mjini.

"Kupita Bambeto kulikuwa jinamizi. Ilikuwa afadhali tutumie nusu saa kuvuka kwa boti kuliko kukwama kwenye foleni ya magari kwa saa mbili. Mara tu barabara hii ya makutano ikifunguliwa, muda wa kusafiri utapunguzwa sana," Sandouno amesema.

Mohamed Cherif Diallo, msimamizi wa wafanyakazi wenyeji wa timu ya mradi huo, ameelezea fahari yake katika mradi huo.

"Makutano ya mzunguko ya Bambeto ni ya kuvutia sana -- ni muundombinu wa kwanza wa ngazi tatu katika historia ya Guinea," amesema. "Tunatumai kuona miradi bora zaidi ya China nchini Guinea katika siku zijazo." ameongeza

Kwa wakazi wa Conakry ambao hupita karibu na mradi huo kila siku, makutano hayo ya barabara hubeba matumaini yao ya maisha bora ya baadaye. Baadhi ya wenye maduka hujitolea kusimamia na kuweka utaratibu mzuri katika eneo la ujenzi, madereva wa teksi hujizoesha na njia mpya za urambazaji, na watoto wanaorudi nyumbani kutoka shuleni hufuatilia maendeleo ya ujenzi wa makutano hayo ya barabara.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha