Kampuni za China zatoa mchango katika soko la ajira la Ethiopia kupitia maonyesho ya kazi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 21, 2025
Kampuni za China zatoa mchango katika soko la ajira la Ethiopia kupitia maonyesho ya kazi
Mwanafunzi wa Ethiopia ajiandikisha na kampuni ya China kwenye shughuli ya maonyesho ya kazi katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mei 19, 2025. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA – Huku msimu wa kuhitimu ukikaribia, Habtamu Tiruneh, mwanafunzi wa mwaka wa tano wa fani ya uhandisi wa mitambo na viwanda katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa (AAU) nchini Ethiopia, amedhamiria kutumia kikamilifu maonyesho ya kazi ya chuo hicho yaliyofanyika kila mwaka ili kupata ajira licha ya changamoto za soko la ajira.

Tiruneh hasa anakusudia kupata nafasi ya kazi au mafunzo ya kazini pamoja na moja ya kampuni kadhaa za China zilizokuwepo kwenye maonyesho hayo, ambayo yamefanyika kuanzia Jumatatu hadi jana Jumanne ikiwa ni sehemu ya Wiki ya Utafiti na Maonyesho ya AAU yenye kaulimbiu ya "Kuongeza Uwezekano wa Kuajirika na Ushirikiano wa Chuo Kikuu na Viwanda."

"Kupata kazi zinazohusiana na nyanja yetu ya masomo imekuwa changamoto siku hizi. Maonyesho ya kazi kama haya yanatumika kama jukwaa muhimu tunapokutana na waajiri watarajiwa moja kwa moja, na pia inajenga imani yetu," Tiruneh ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua alipokuwa akikaribia banda la kampuni ya ujenzi ya China.

Katika maonyesho hayo, kampuni za China zinazojihusisha na sekta muhimu za maendeleo ya Ethiopia -- kuanzia miundombinu hadi TEHAMA -- zimevutia wimbi la watu wanaotafuta kazi walio na shauku.

Shirika la Uhandisi wa Ujenzi la China (CCECC), shirika kubwa la ujenzi ambalo limekuwa likifanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa zaidi ya muongo mmoja, ni moja ya kampuni 20 za China zilizoshiriki kwenye maonyesho hayo ya kazi.

Likiwa na wafanyakazi wenyeji takriban 5,000 nchini Ethiopia, CCECC inalenga kuimarisha zaidi timu yake ya nchini humo kwa kuajiri wahitimu wapatao 40 kutoka kwenye maonyesho hayo kwa nafasi, zikiwemo za wahandisi, wahasibu, wasimamizi wa masoko na watafsiri.

"Kampuni za China ni mashuhuri katika miundombinu, viwanda na sekta zingine za Ethiopia," Tiruneh amesema. "Ninaamini kwamba kufanya kazi kama mhandisi mdogo wa mitambo na viwanda katika moja ya kampuni hizi itakuwa fursa nzuri kwa maendeleo yangu ya kikazi ya baadaye, hasa kwa sababu ya ujuzi wao wa kina na teknolojia ya hali ya juu."

Takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ujuzi ya Ethiopia zinaonyesha kuwa hali ya kutowiana kati ya mahitaji ya wafanyakazi na usambazaji ni changamoto kubwa katika soko la ajira la Ethiopia, huku idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi nchini humo ikikadiriwa kuwa milioni 60.

Akihimiza taasisi za elimu na kampuni kuwekeza katika kuziba pengo hilo, Solomon Addis, mtaalamu wa mfumo wa taarifa za soko la ajira katika wizara hiyo, amesisitiza jukumu muhimu la maonyesho ya kazi katika kuunganisha nguvu kazi na kampuni.

"Maonyesho ya leo ya kazi yanaangazia suala muhimu katika nchi yetu, kuhusu kudorora kwa fursa za ajira na ukosefu wa imani walionao waajiri kwa wahitimu wapya," amesema Kassu Jilcha, mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo ya Kazi ya Wanafunzi katika AAU.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha