Maonyesho ya kimataifa eneo la magharibi mwa China yavutia kampuni zaidi ya 3,000

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 26, 2025
Maonyesho ya kimataifa eneo la magharibi mwa China yavutia kampuni zaidi ya 3,000
Hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 20 ya Kimataifa ya Eneo la Magharibi mwa China ikifanyika mjini Chengdu, Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China, Mei 25, 2025. (Xinhua/Liu Kun)

CHENGDU - Maonyesho ya 20 ya Kimataifa ya Eneo la Magharibi mwa China (WCIF) yamefunguliwa rasmi jana Jumapili huko Chengdu, mji mkuu wa Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, yakionyesha teknolojia mpya za kisasa na bidhaa mbalimbali, yakivutia kampuni zaidi ya 3,000 kutoka nchi na maeneo 62 kushiriki kwenye maonesho hayo.

Kwa mara ya kwanza, maonyesho hayo ya mwaka huu yana nchi mbili wageni waheshimiwa: Laos na Hungary. Banda la Laos linaonyesha bidhaa za chai, kahawa, samani na kazi za mikono, huku Banda la Hungary likiwasilisha kampuni 17 zilizobobea katika mvinyo, zana za matibabu na teknolojia ya kutibu maji ambayo ni rafiki kwa mazingira.

"Maonyesho hayo yanatoa fursa ya thamani kwa uunganishaji wadau wa biashara, ushirikiano katika uwekezaji na upashanaji habari kampuni za viwanda kutoka Laos na nchi nyingine, na kuimarisha kwa ufanisi mafungamano na utandawazi katika masoko ya bidhaa za kikanda," Naibu Waziri Mkuu wa Laos Kikeo Khaykhamphithoune amesema kwenye hafla ya ufunguzi.

Akiwa anashiriki kwa mara ya kwanza kwenye maonyesho hayo, mfanyabiashara wa Indonesia Fransisca Pauline Tjandra anaonyesha vitu vilivyotengenezwa kwa mikono. Na kwa kuendesha warsha juu ya kazi za mikono kama vile shanga za magamba ya viumbe vya baharini, anatarajia kwamba Wachina zaidi watajifunza kuhusu kazi za mikono za Indonesia kupitia maonesho hayo.

"Kwa kushiriki kwenye maonyesho haya, hata nimejifunza maneno ya Kichina yanayotumia kila mara , kama vile 'nihao' (hujambo), 'xiexie' (shukrani) na 'Duoshaoqian?' (pesa ngapi? )," amesema.

Yakiwa yameandaliwa na serikali ya mkoa wa Sichuan, Maonyesho hayo yamepangwa kufanyika hadi Alhamisi wiki hii. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha