

Lugha Nyingine
China na Indonesia zasisitiza tena Moyo wa Bandung, na kuahidi ushirikiano wa karibu
![]() |
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akifanya mazungumzo na Rais wa Indonesia Prabowo Subianto kwenye Ikulu ya Merdeka mjini Jakarta, Indonesia, Mei 25, 2025. (Xinhua/Liu Weibing) |
JAKARTA – Katika ziara rasmi ya Waziri Mkuu wa China Li Qiang nchini Indonesia, nchi hizo mbili zimeangazia thamani ya Moyo wa Mkutano wa Kihistoria wa Bandung katika zama ya sasa na kuahidi ushirikiano wa karibu zaidi wa pande mbili pamoja na uratibu bora wa kimkakati.
"China inapenda kushirikiana na Indonesia na nchi nyingine zinazoendelea ili kwa pamoja kushikilia Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani na Moyo wa Bandung," Waziri Mkuu Li amesema jana Jumapili kwenye mazungumzo na Rais wa Indonesia Prabowo Subianto.
Aprili 1955, mkutano wa kihistoria katika mji wa Bandung nchini Indonesia ulikusanya nchi 29 za Asia na Afrika chini ya bendera ya mshikamano, urafiki na ushirikiano, ikimaanisha mwanzo wa mwamko wa sehemu ya dunia inayojulikana sasa kama kundi la Nchi za Kusini.
"Leo, zaidi ya miongo saba baadaye, dunia kwa mara nyingine iko katika njia panda muhimu," Waziri Mkuu Li alisema Jumamosi alipokuwa akihutubia jumuiya ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.
“Hali ya upande mmoja na kujilinda kibiashara kunaongezeka, na vitendo vya umwamba vinaongezeka,” alisema, akisisitiza kwamba dhidi ya hali hiyo, thamani ya zama za sasa ya Moyo wa Bandung imekuwa muhimu zaidi.
Muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Li kuwasili juzi Jumamosi, Li na Rais Prabowo kwa pamoja walitembelea maonyesho ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kufanyika kwa Mkutano huo wa Bandung.
Katika ziara yake hiyo, Waziri Mkuu Li amezihimiza China na Indonesia kupanua ushirikiano zaidi, kuimarisha mafungamano ya kiviwanda na kulinda biashara huria.
Amemwambia Prabowo jana Jumapili kwamba China inapenda kushirikiana na Indonesia ili kuimarisha kuunganisha mikakati ya maendeleo ya nchi mbili na kuzidisha ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, hasa kwa kuboresha na kuimarisha miradi muhimu. Amezihimiza pande hizo mbili kuboresha zaidi "chapa ya dhahabu" ya Reli ya Mwendokasi ya Jakarta-Bandung.
Waziri Mkuu huyo pia amesema pande zote mbili zinapaswa kuimarisha muunganisho wa soko na ushirikiano wa kiviwanda, kuboresha kiwango cha uwezeshaji wa biashara na uwekezaji, na kupanua ushirikiano katika maeneo kama vile mambo ya fedha, nishati mpya, uchumi wa kidijitali, akili mnemba (AI), anga ya juu na bahari.
Akibainisha kuwa mwaka 2025 ni maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili na maadhimisho ya miaka 70 tangu kufanyika Mkutano wa Bandung, Rais Prabowo amesema Jumapili kwamba Indonesia itachukua fursa hiyo kuzidisha ushirikiano wa kimkakati wa pande zote na China na kwa pamoja kuhimiza amani, maendeleo barani Asia na duniani.
Amesema Indonesia inapenda kupanua ushirikiano na China katika kilimo, mambo ya fedha, ujenzi wa miundombinu, uchumi wa kijani, AI na elimu, na kuboresha ushirikiano wa kiviwanda. Rais Prabowo pia ameelezea matumaini kwamba kampuni zaidi za China zitawekeza na kufanya biashara nchini Indonesia.
Viongozi hao wawili Jumapili walishuhudia utiaji saini wa nyaraka kadhaa za ushirikiano katika maeneo yanayohusu sera za maendeleo ya kiuchumi, mnyororo wa viwanda na mnyororo wa usambazaji vilevile mambo ya fedha.
Waziri Mkuu Li pia alikutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Indonesia Puan Maharani jana Jumapili.
Shughuli za kiutamaduni zafanyika kwenye Jukwaa la Russia na China mjini Khabarovsk, Russia
Miti ya jacaranda katika mchanuo wa maua yavutia watalii mjini Kunming, China
Upandaji mahindi waingia kipindi cha kilele katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, China
UNESCO latoa wito upya wa kuimarishwa ulinzi wa maeneo ya urithi ya Afrika
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma